Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Monday, May 14, 2012

Kuenea chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani

Kuenea chuki dhidi ya Uislamu nchini Marekani sambamba na kupanuka wigo wa kukanyagwa haki za Waislamu katika nchi hiyo ni mambo ambayo yamekuwa yakichukua mkondo mpya kila siku. Hii ni katika hali ambayo, propaganda kama hizi za chuki dhidi ya Uislamu ambazo zimekuwa zikiakisiwa kila leo na vyombo vya habari vya Marekani, zimepelekea kushtadi vitendo vya utumiaji mabavu dhidi Waislamu katika nchi hiyo. Pamoja na hayo, chuki dhidi ya Uislamu hazijaishia tu katika vyombo vya habari vya Marekani. 

Baadhi ya waumini wa Kiislamu wakiwa katika midahalo yao
Katika uga huo, Baraza la Mahusiano ya Uislamu na Marekani limeanzisha masomo ya chuki dhidi ya Uislamu kwa ajili ya wanajeshi wa Kimarekani. Mafundisho hayo yanaiarifisha dini ya Kiislamu kuwa adui halisi wa Marekani. Aidha wanajeshi hao wa Marekani wanafundishwa katika masomo hayo kwamba, wanapaswa kuilenga kwa mabomu ya atomiki miji ya Makka na Madina kama ilivyokuwa kwa mji wa Hiroshima. Baada ya kufichuliwa masomo hayo, viongozi wa Marekani wamejitoa kimasomaso na kutangaza kwamba, masomo hayo yamesimamishwa na eti uchunguzi juu ya suala hilo unaendelea. Licha ya matamshi hayo ambayo lengo lake ni kutaka kujikosha lakini walimwengu wangali wanashuhudia vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo. Ni hivi karibuni tu ambapo kasisi mwenye kufurutu ada Terry Jones wa Florida huko Marekani alikariri tena kitendo chake cha kishenzi cha kuchoma moto Qur'ani. Picha za hatua hiyo ya uchomaji moto Qur'ani zilionyeshwa moja kwa moja katika kanali ya intaneti. Licha ya kuwa wakati anaingia madarakani, Rais Barack Obama wa Marekani aliahidi kwamba, angebadilisha muamala wa Washington dhidi ya Waislamu, lakini kutokea vitendo vyote hivi vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani, kumethibitisha wazi kwamba, rais huyo amekwenda kinyume kabisa na ahadi yake.
Ukweli wa mambo ni kuwa, viongozi wa ngazi za juu wa Marekani wamekuwa wakitumia kisingizio cha uhuru wa mtu binafsi hususan uhuru wa kutoa maoni, kutozuia vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Hii ni katika hali ambayo, kuhusiana na suala la holocaust hali ya mambo ni kinyume kabisa nchini Marekani na Ulaya kwa ujumla; kwani anayekana au kutilia shaka holocaust hukabiliwa na adhabu kali kabisa. Inavyoonekana ni kuwa, propaganda za chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu ambazo zilianza baada ya matukio ya Septemba 11 mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi sasa zimechukua mkondo mpya na mpana zaidi.

No comments: