Msemaji wa polisi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo amesema kuwa, vikosi vya polisi vimekabiliana na wapinzani wa
serikali na kusababnisha mtafaruku mkubwa.
Kanali Mwana Mputu ametangaza
kuwa, makabaliano hayo yametokea katika mji mkuu Kinshasa kati ya vikosi
vya polisi na wapinzani ambao ni wafuasi wa chama cha UDPS
kinachoongozwa na Etienne Tshisekedi.
Augustin Kabuya Naibu msemaji wa chama
cha mwanasiasa mkongwe wa DRC Etienne Tshisekedi cha UDPS amesema kuwa,
vurugu kati ya polisi na wafuasi wa chama hicho zilianza baada ya
mwanaharakati mmoja wa chama hicho kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Akizungumzia vurugu hizo, msemaji wa
polisi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, vikosi vyao
vililazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa chama
hicho.
Amesema, polisi katika jiji la Kinshasa imefanikiwa kurejesha amani
na utulivu ingawa vurugu hizo zimesababisha hasara ikiwemo ya kuchomwa
moto basi moja.
Aidha amesema kuwa, askari
aliyemfyatulia risasi na kumuua raia huyo tayari ametiwa mbaroni na
atapandishwa kizimbani katika mahakama ya kijeshi.
Katika siku za hivi karibuni Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikishuhudia maandamano ya mara kwa mara
yanayoipinga serikali ya Rais Joseph Kabila.
Rais Kabila anayemaliza muhula wake wa uongozi mwaka huu, amekuwa
akitoa wito mara kwa mara wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa, wito ambao
umekuwa ukipingwa na wapinzani.
Wapinzani wanasema kuwa, lengo la
mazungumzo hayo ni njama ya serikali kutaka kuakhirisha uchaguzi wa rais
wa Novemba mwaka huu na hivyo kuongeza muda wa Rais Kabila kuendelea
kuweko madarakani.
Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, uchaguzi wa
rais unapaswa kufanyika mwezi Novemba ambapo Rais Kabila hapaswi kuwania
kiti hicho kwa muhula mwingine.
No comments:
Post a Comment