Waasi watiifu kwa Riek Machar, makamu wa zamani wa Rais wa Sudan
Kusini wamesema kuwa wameuteka mji unaozalisha mafuta kwa wingi wa
Malakal baada ya mapigano ya siku tatu na vikosi vya serikali ya juba.
Moses Ruai Lat msemaji wa waasi watiifu kwa Machar amesema leo kuwa mji wote wa Malakal unadhibitiwa na vikosi vyao.
Hata hivyo Kuol Manyang Juuk, Waziri wa Ulinzi wa Sudan Kusini
amepinga madai hayo ya waasi watiifu kwa Machar akisema kuwa ni ya
uwongo.
Amesema wapiganaji watiifu kwa Riek Machar wamepata kipigo na
hawapo tena katika mji huo mkubwa kwa uzalishaji wa mafuta. Waziri wa
Ulinzi wa Sudan Kusini amesema kuwa mji wa Malakal unadhibitiwa
kikamilifu na majeshi ya serikali.
Wakatihuohuo, nchi jirani na Sudan Kusini leo zimemuunga mkono Rais
Salva Kiir wa nchi hiyo baada ya siku 13 za mapigano katika nchi hiyo
changa zaidi duniani. Nchi jirani na Sudan Kusini zimesema kuwa
hazitakubali hatua yoyote ile ya kumuondoa madarakani Rais Kiir na
serikali yake iliyochaguliwa kwa njia ya kidemokrasia.
Nchi za Magharibi na zile za za Kiafrika zinahofia kuwa mapigano
yanayoendelea kati ya vikosi vya serikali na waasi watiifu kwa makamu wa
zamani wa Rais Salva Kiir yaani Riek Machar yanaweza kuchochea vita vya
ndani vya kikabila ambavyo vitakuwa hatari kwa nchi za eneo hilo.
Akihutubia viongozi wa kieneo katika mkutano wa dharura ulioitishwa
huko Juba na Jumuiya ya Igad kujadili mgogoro wa Sudan Kusini, Rais
Uhuru Kenyatta wa Kenya amewataka Kiir na Machar kutumia fursa iliyopo
na kuanza mazungumzo ya amani.
No comments:
Post a Comment