Idadi ya wahanga wa shambulizi la jana la kundi la Boko Haram
katika mpaka wa Nigeria na Cameroon, imeongezeka na kufikia watu 42. Kwa
mujibu wa habari zilizothibitishwa na maafisa usalama nchini Nigeria,
watu wasiopungua 42 waliuawa katika shambulizi hilo jipya lililofanywa
na wanachama wa kundi hilo katika vijiji vya Kanari, Wazarde na Gula
katika jimbo la Borno, la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Inaelezwa
kuwa vijiji hivyo viko katika eneo la Gamboru karibu na mpaka wa nchi
hiyo na Cameroon ambapo mwanzoni mwa mwezi uliopita kundi hilo lilifanya
mauaji ya kutisha dhidi ya watu wasiopungua 300.
Mashuhuda wameeleza kuwa, watu wenye silaha wanaosadikiwa kuwa
wanachama wa Boko Haram na ambao walikuwa katika malori yaliyokuwa
yamebeba silaha na mada za miripuko walivamia vijiji hivyo na
kuviteketeza kwa moto, ambapo mbali na kuua idadi kubwa ya watu,
walijeruhi mamia ya wengine. Mashambulizi hayo yaliendelea kwa muda
usiopungua masaa saba, na cha kushangaza ni kuwa hakuna askari yeyote wa
serikali aliyefika eneo hilo. Hali hiyo imewafanya asilimia kubwa ya
Wanigeria kuamini kuwa mashambulizi hayo yanafanyika kwa baraka za
maafisa usalama wa nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment