Abdul Fattah al Sisi, kiongozi wa kijeshi aliyeongoza mapinduzi
ya kijeshi dhidi ya rais aliyechaguliwa na wananchi Muhammad Mursi,
ataapishwa siku ya Jumamosi ijayo kama rais mpya wa Misri. Duru za
habari zimewanukuu maafisa wa vyombo vya mahakama nchini Misri wakisema
leo kwamba, tume ya uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni nchini
humo, itatangaza matokeo rasmi ya uchaguzi huo siku ya Jumanne.
Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa matokeo yasiyo rasmi ya
uchaguzi huo, kiongozi huyo wa kijeshi na waziri wa zamani wa ulinzi wa
nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, ameshinda kwa zaidi ya asilimia 93 ya
kura.
Uchaguzi wa rais nchini Misri ulifanyika wiki iliyopita kwa
ushiriki dhaifu wa wananchi baada ya kususiwa na vijana walio wengi
ambao ndio walioongoza harakati za mapinduzi dhidi ya utawala wa dikteta
Hosni Mubarak mwaka 2011.
Wakati huo huo mahakama moja nchini Misri leo imesikiliza kesi ya
Mubarak na wanawe wawili Alaa na Gamal katika kesi maarufu inayoitwa
'kesi ya karne' ambapo watuhumiwa hao walifikishwa kizimbani. Katika
kesi hiyo Mubarak na wanawe wanatuhumiwa kufanya mauaji dhidi ya
waandamanaji katika maandamano ya amani na pia kutokana na kuiingizia
hasara ya mabilioni ya fedha Misri kutokana na kuuzia utawala haramu wa
Kizayuni gesi ya nchi hiyo kwa bei ya kutupa.
No comments:
Post a Comment