Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Monday, June 2, 2014

Iran na Kuwait kuimarisha uhusiano katika nyanja zote

Rais Hassan Rouhani wa Iran leo amemfanya mazungumzo na mgeni wake Sheikh Sabah Al Ahmad Al Jaber Al Sabah Amir wa Kuwait mjini Tehran na kusisitiza juu ya kuimarishwa mashirikiano ya pande mbili katika nyanja zote. Baada ya kumalizika duru ya kwanza ya mazungumzo ya pande mbili, Iran na Kuwait zilitiliana saini hati sita za makubaliano ya pande mbili katika nyanja za usalama, ushuru wa forodha, uchukuzi wa anga, utalii, hifadhi ya mazingira na michezo.
Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa, suala la kuimarishwa uhusiano na Kuwait katika nyanja zote, linapewa kipaumbele katika sera za kigeni za Iran.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumlaki Sheikh Sabah Al Ahmad Al Jaber Al Sabah Amir wa Kuwait katika uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran, Dakta Muhammad Javad Zarif ameongeza kuwa, safari ya Amir wa Kuwait itaanza kufungua ukurasa mpya wa kuimarishwa mashirikiano ya nchi hizo mbili. Dakta Zarif ameeleza kuwa, safari iliyopangwa kufanyika hivi karibuni nchini Saudi Arabia imeakhirishwa kutokana na safari hiyo kuingiliana na ratiba za  mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran ameeleza kuwa,  mazungumzo ya mara kwa mara ya nyuklia yatapelekea kufikiwa makubaliano ya mwisho na kusisitiza kwamba nchi za Magharibi zilijaribu kutumia mbinu mbalimbali kama vile vikwazo, mashinikizo na vitisho lakini hakuna hata mbinu moja iliyoweza kuwafikisha kwenye malengo yao haramu, bali  zinazidi  kuwa mbali na malengo yao siku hadi siku.

No comments: