Feisal Miqdad, Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Syria
amezikosoa vikali baadhi ya nchi za Magharibi na Kiarabu kwa kuwazuia
wananchi wa Syria wanaoishi kwenye nchi hizo, kushiriki katika zoezi la
kupiga kura kwenye uchaguzi wa rais wa nchi hiyo. Feisal Miqdad
ameongeza kuwa, baadhi ya nchi kama vile Ufaransa, Ubelgiji, Ujerumani
na Bulgaria ambazo hujinadi kutetea misingi ya demokrasia zimewazuia
Wasyria kushiriki kwenye uchaguzi huo. Ameongeza kuwa, baadhi ya nchi za
Kiarabu nazo pia ziliamua kuchukua maamuzi hayohayo dhidi ya Syria
ambayo yanakinzana na sheria za kimataifa kutokana na kuhofia
mashinikizo kutoka Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi
Arabia.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ameongeza kuwa, nchi hizo
zimekiuka makubaliano ya mahusiano ya kidiplomasia ya 'Vienna'. Miqdad
amebainisha kuwa, madai ya nchi hizo ya kutetea demokrasia na misingi ya
haki za binadamu ni uwongo. Feisal al Miqdad ameikosoa serikali ya
Ufaransa kutokana na misimamo yake ya kiadui na chuki dhidi ya Syria na
kusisitiza kwamba, Paris imepoteza uhalali wake wa kimataifa, kwani
katika uchaguzi wa Bunge la Ulaya uliofanyika tarehe 25 mwezi uliopita,
chama tawala cha Ufaransa kilishindwa vibaya kwenye uchaguzi huo na
wananchi wengi wa nchi hiyo wanataka yafanyike mabadiliko ya viongozi
nchini humo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ameongeza kuwa, serikali ya
Damascus haiingilii mambo ya ndani ya Ufaransa, lakini Wafaransa
wamekuwa na tabia ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu
kwa kuwaunga mkono magaidi, ambao wanatenda jinai za kivita na
kibinadamu nchini humo.
No comments:
Post a Comment