Huku machafuko yakizidi kushika kasi nchini Jamhuri ya Afrika ya
Kati, kwa mara nyingine tena, waasi wa Kikristo wa Anti-Balaka wamevamia
msikiti mmoja mjini Bangui na kuuharibu kabisa. Hii ni katika hali
ambayo hivi karibuni pia kanisa moja mjini humo lilishambuliwa na watu
wenye silaha wanaosadikiwa kuwa na mafungamano na waasi hao na kufanya
mauaji dhidi ya watu wasiopungua 30 akiwemo padri wa kanisa hilo.
Kufuatia kuongezeka wimbi la vitendo vya ukatili nchini humo, Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa, sambamba na kutoa tamko kuhusiana na suala
hilo, limeyataka makundi yanayohusika katika vitendo hivyo, kuweka chini
silaha na kufuata mkondo wa amani nchini humo.
Katika ripoti hiyo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitaka
serikali ya Rais Catherine Samba-Panza wa Jamhuri ya Afrika ya kati,
kuwachukulia hatua kali na za haraka wahusika wa vitendo hivyo. Vile
vile Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR
amelaani shambulizi hilo dhidi ya kanisa mjini Bangui, na kuyataja
machafuko hayo ya hivi karibuni kuwa ni dalili za kuzorota hali ya
usalama nchini humo. Adrian Edwards amelaani mashambulizi dhidi ya
maeneo ya ibada ambayo ndio maeneo yaliyosalia kwa ajili ya kuwahifadhi
wakimbizi na kutaka kukomeshwa mashambulizi hayo mara moja. Hayo
yanajiri katika hali ambayo, wakazi wa mjini Bangui, wamefanya
maandamano makubwa mjini humo wakimtaka Rais Panza ajiuzulu kutokana na
kile wanachodai kuwa ni kushindwa serikali yake ya mpito kumaliza
machafuko nchini mwao.
Kwa upande mwingine baada ya kushambuliwa kanisa mjini Bangui, Rais
Catherine Samba-Panza aliwahutubia wananchi na kulaani vikali tukio hilo
aliloliita kuwa la kigaidi. Aidha alionyesha kusikitishwa kwake na
ongezeko la vitendo vya ukatili mjini Bangui na kuenea vitendo hivyo
katika maeneo mengine ya nchi hiyo. Amesema jambo hilo linatishia
usalama wa taifa zima. Hata hivyo kile kinachowashangaza wengi ni
radiamali ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na kujaribu kwao
kufunika ukweli wa matukio ya hivi karibuni nchini humo. Hii ni katika
hali ambayo shambulizi dhidi ya kanisa hilo limeakisiwa kwa upana mno
katika vyombo vya habari vya Magharibi, huku shambulizi dhidi ya msikiti
likiwa limepuuzwa kabisa.
Kabla ya hapo pia Waislamu wengi waliuawa na kujeruhiwa katika
mashambulizi ya waasi hao wa Kikristo wa Anti-Balaka katika misikiti
kadhaa nchini humo. Waasi hao walianzisha mashambulizi yao ya kidini
dhidi ya Waislamu tangu mwezi Disemba mwaka jana. Ripoti zinasema kuwa,
tangu kuanza machafuko hayo ya ndani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati,
zaidi ya watu milioni moja yaani karibu robo nzima ya wananchi wa nchi
hiyo ya katikati mwa Afrika, wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.
Kabla ya hapo pia na kufuatia kushadidi mapigano ya kikaumu na
kuongezeka machafuko nchini humo, viongozi wa Kiislamu na wale wa
Kikristo walitangaza umoja kati ya wafuasi wa dini hizo. Hata hivyo
juhudi hizo hazikuweza kupunguza machafuko nchini humo. Kwa upande
mwingine, mapigano ya kikaumu nchini humo yanajiri mbele ya macho ya
maelfu ya askari wa kimataifa wa kulinda amani wakiwemo wale wa
Ufaransa. Kuwepo askari hao nchini humo, hakujasaidia lolote katika
kuzuia mauaji ambayo Waislamu ndio wahanga wake wakuu wa machafuko hayo.
No comments:
Post a Comment