Naibu Waziri wa Usalama wa Taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
ametangaza, kutiwa mbaroni magaidi 30 wa mtandao wa al-Qaida nchini
hapa. Ali Khazai aliyasema hayo hapo jana kabla ya hotuba ya sala ya
Ijumaa iliyosaliwa mjini Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran na
kuongeza kuwa, wanachama wa mtandao huo wa kigaidi, wametiwa mbaroni na
askari wa usalama katika miezi ya hivi karibuni.
Akiashiria kwamba,
tangu tukio la Septemba 11 hapo mwaka 2001 nchini Marekani, daima Wizara
ya Usalama ya Iran imekuwa ikifuatilia kwa karibu nyendo za mtandao wa
al-Qaida hapa nchini, Khazai ameongeza kuwa, makundi ya kigaidi hayaachi
kufanya njama za kigaidi na uvurugaji wa usalama hasa katika maeneo
matakatifu. Ameashiria jinai za makundi hayo likiwemo kundi la Dola la
Kiislamu la Iraq na Sham kwa kifupi Daesh katika nchi za Kiislamu kama
Iraq na Syria na kusema, mashambulizi ya makundi hayo yanatekelezwa kwa
msaada na himaya kamili ya Marekani na utawala haramu wa Israel. Naibu
Waziri wa Usalama wa Taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza
kuwa, makundi ya kitakfiri na Daesh hayana uhasama na uadui na watu wa
madhehebu ya Kishia peke yao, bali ni maadui na watu wa madhehebu ya
Kisuni na kwamba mfano ulio wazi kuhusu suala hilo ni hujuma na jinai za
hivi karibuni zilizofanywa na kundi hilo mjini Mosul, Iraq. Amesisitiza
kuwa, Mashia kwa kushirikiana na wenzao Ahlu Sunna wal-Jamaa lazima
waungane katika kukabiliana na makundi ya Kiwahabi na masalafi wa
kitakfiri katika kila sehemu ya dunia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment