Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, May 20, 2014

Wasiwasi wa kuporomoka satua ya Marekani kimataifa

Kuendelea kuvurunda serikali ya Marekani katika masuala mbalimbali ya kimataifa kumewafanya wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa wa nchi hiyo kuingiwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa kisiasa, kijeshi na kiuchumi wa nchi yao. Gavana wa jimbo la New Jersey, Chris Christie amenukuliwa akisema kuwa, Marekani imepoteza ushawishi wake na kwa sasa nchi hiyo haiko kwenye nafasi ya kwanza katika orodha ya nchi zenye satua na nguvu kubwa duniani. Gavana wa New Jersey anailaumu serikali ya Rais Barack Obama na sera zake za nje akisema ikulu ya White House imepoteza dira na kwa mantiki hiyo, mustakabali wa Marekani kimataifa unakumbwa na atiati.
Kuna uwezekano mkubwa Chris Christie akawania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2016 kwa tiketi ya chama cha Republicans. Mwanasiasa huyo anasema zama za Rais Ronald Regan Marekani ilikuwa na nguvu na satua katika kila nyanja na kwamba iliweza kuainisha marafiki na maadui zake lakini satua hiyo imefifia na inakabiliwa na hatari ya kutoweka katika siku za usoni.
Matamshi ya Gavana wa New Jersey yanahesabiwa kuwa sehemu ya mashindano ya kisiasa kati ya vyama vya Republicans na Democrats kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Kwa mtazamo wa chama cha upinzani cha Republicans na pia idadi kubwa ya wadau na wafuasi wa chama tawala cha Democrats ni kwamba, kuanzia muongo wa 50 hadi 80, Marekani ilikuwa na uwezo mkubwa na kwa mahesabu ya haraka Washington ilikuwa ikitawala zaidi ya asilimia 50 ya dunia. Wakati huo viongozi wa Marekani walifanya chochote walichokitaka kwa njia ya moja kwa moja au kupitia waitifaki wao bila matatizo yoyote. Marekani kupitia njia hiyo iliweza kuwashinikiza viongozi mbalimbali waliokuwa wakipinga mfumo wake wa kibeberu na pale mashinikizo yalipoonekana kutozaa matunga basi Washington iliweza kuwapindua na kuwaondoa madarakani viongozi hao kwa kutumia nguvu za kijeshi za moja kwa moja au kupitia waitifaki wake.
Kwa sasa mambo yamebadilika na hali hiyo haipo tena. Mambo mengi yamepelekea kudhoofika satua ya Marekani kimataifa hususan katika kipindi cha utawala wa George W. Bush wa chama cha Republicans na Rais Barack Obama kutoka Democrats. Wachambuzi wengi wanaamini kuwa, matukio ya miaka ya hivi karibuni kama vile uvamizi wa Marekani nchini Iraq kinyume na sheria za kimataifa, ujasusi wa kupindukia wa Washington dhidi ya nchi na viongozi mbalimbali wa dunia hata wale wanaodaiwa kuwa ni waitifaki wake, ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wa Marekani katika jela za Abu Ghureib na Guantanamo ni miongoni mwa mambo yanayoifanya nchi hiyo kupoteza umashuhuri kwa kasi ya ajabu.  
Tangu mwishoni mwa karne ya 20 dalili za kuporomoka satua ya Marekani kimataifa zilikua zimeanza kuonekana na hata baadhi ya weledi wa mambo wakatabiri kwamba Washington itapoteza uwezo wake wa kiuchumi na kijeshi duniani kwa mataifa kama vile China na Japan. Utabiri huo unaelekea kutimia kwani kwa sasa nchi hiyo inakabiliwa na madeni chungu nzima na takwimu zinaonyesha kuwa madeni hayo yamepindukia dola trilioni 17

No comments: