Waislamu nchini Nigeria wameeleza kuchukizwa kwao na vitendo
vinavyoendelea kufanywa na kundi la Boko Haram la nchi hiyo na kulaani
vikali kuhusishwa vitendo hivyo vichafu na dini tukufu ya Kiislamu.
Waislamu nchini Nigeria jana walikusanyika katika Msikiti Mkuu wa Abuja
na kumuomba Mwenyezi Mungu ili wasichana zaidi ya 250 wanaoshikiliwa
mateka na kundi la Boko Haram waachiliwe huru. Sheikh Mussa Muhammad
Imam wa msikiti huo amesema kuwa, dini ya Kiislamu inapinga vikali
kitendo cha kuwaua watu wasio na hatia.
Sheikh Mussa Muhammad ameongeza
kuwa, dini tukufu ya Kiislamu pia haimlazimishi mtu kufuata dini hii
bila ya ridhaa yake. Imam wa Msikiti Mkuu wa Abuja amesema kuwa, kundi
la Boko Haram haliwalengi na kuwaua Wakristo pekee, bali hata Waislamu
wamekuwa wakiuawa na kushambuliwa na kundi hilo. Waislamu waliokusanyika
jana kwenye Msikiti Mkuu wa Abuja wamesema kuwa, kundi la Boko Haram
linatafsiri visivyo Qurani Tukufu na Jihadi, na kwamba vitendo
vinavyofanywa na kundi hilo ikiwa ni pamoja na kuwaua watu wasio na
hatia, uripuaji na uchomaji moto nyumba za wanavijiji, ni kinyume na
mafundisho ya dini ya Kiislamu. Inafaa kuashiria hapa kuwa, miaka kadhaa
iliyopita, maulamaa kadhaa wa Kiislamu waliuawa kinyama baada ya
kulikosoa kundi hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment