Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Tuesday, May 20, 2014

Shambulio la al Shabab laua askari 12 nchini Kenya

Askari  usalama wasiopungua 12  wa Kenya wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya wanamgambo wa al Shabab kuushambulia msafara wa askari  hao  uliokuwa ukitoka katika mji wa Maua na kuelekea kwenye Kaunti ya Mandera iliyoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Noah Mwivanda, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Mandera amethibitisha taarifa za kutokea shambulio hilo na kusema kwamba, maafisa wengine wanne wa KPR wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo na wanapatiwa matibabu kwenye hospitali ya Mandera. Wakati huohuo,Serikali ya Kenya imetangaza kuimarisha zaidi ulinzi na usalama karibu na majengo ya balozi za kigeni, majengo ya jumuiya za kimataifa, majengo ya serikali na kwenye miundombinu muhimu ya nchi hiyo ili kukabiliana na tishio la kutokea mashambulio ya kigaidi katika mji mkuu wa nchi hiyo Nairobi. Polisi ya Kenya imetangaza kuwa, ulinzi mkali umewekwa kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi na abiria wote wanaoingia wanapaswa kukaguliwa kikamilifu. Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kutolewa indhari ya tishio la mashambulizi ya kigaidi nchini humo. Inafaa kuashiria hapa kuwa, katika wiki za hivi karibuni Kenya imekuwa ikishuhudia miripuko ya mara kwa mara inayofanyika hasa kwenye mabasi ya abiria na kusababisha makumi ya watu kuuawa na kujeruhiwa.

No comments: