Rais wa Marekani ameliandikia barua Baraza la Kongresi la nchi hiyo juu
ya mpango wa kutumwa wataalamu 80 wa kijeshi wa nchi hiyo huko Chad. Kwa
mujibu wa madai ya Rais Barack Obama, wanajeshi hao wa Marekani
watapelekwa nchini Chad kwa shabaha ya kuisaidia serikali ya Nigeria
kwenye operesheni ya kuwaokoa wanafunzi wasichana 276 wanaoshikiliwa
mateka na wanamgambo wa kundi la Boko Haram la nchi hiyo. Kundi la Boko
Haram liliwateka nyara wanafunzi hao wa shule ya bweni kwenye mji wa
Chibok ulioko kwenye jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa nchi hiyo
mwezi uliopita. Wanamgambo hao walitishia kwenye mkanda wa video
waliourusha hewani kwamba, watawauza kama vijakazi wasichana hao kwenye
nchi za Cameroon na Chad. Serikali ya Nigeria kuanzia mwezi Mei mwaka
jana ilitangaza hali ya hatari kwenye majimbo manne yaliyoko kaskazini
mashariki mwa nchi hiyo, kwa shabaha ya kupambana na kundi hilo. Hadi
sasa operesheni za kigaidi katika maeneo hayo zingali zinaendelea na
kusambaa hadi Abuja, mji mkuu wa Nigeria. Mara baada ya kutekwa nyara
wanafunzi hao, serikali ya Nigeria haikuchukua hatua zozote muhimu za
kuwakomboa wanafunzi hao, hadi pale wananchi walipoandamana na kupasa
sauti zao zilizosikika pembe mbalimbali ulimwenguni kupitia mitandao ya
kijamii. Hii ni katika hali ambayo, licha ya kutekwa nyara wanafunzi
hao, miripuko ya mabomu iliyotokea hivi karibuni katika mji wa Jos na
kupelekea watu wasiopungua 150 kuuawa, imeandaa mazingira kwa madola ya
Magharibi kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo. Rais Francois
Hollande wa Ufaransa wiki iliyopita kwa kutumia kisingizio cha masuala
ya kibinadamu, aliitisha kikao mjini Paris, kilichowashirikisha wakuu wa
nchi za Nigeria, Niger, Cameroon, Chad na Benin kwa lengo la kujadili
usalama wa Magharibi mwa Afrika na hasa kuhusiana na kadhia ya kutekwa
nyara wanafunzi wasichana nchini Nigeria. Kwenye mazungumzo hayo, Rais
Hollande alitahadharisha juu ya kutokea vita barani Afrika
vitakavyosababishwa na jinai za kigaidi za Boko Haram. Rais wa Ufaransa
amewaomba wakuu wa nchi tano za Kiafrika zinazopakana na Nigeria,
watekeleze operesheni za pamoja kwa lengo la kuliangamiza kundi hilo.
Vyovyote itakavyokuwa, serikali ya Nigeria haiwezi kulitokomeza kundi la
Boko Haram, bila ya kushirikiana kijeshi na kiusalama na nchi majirani.
Lakini hivi sasa, serikali ya Nigeria iko ukingoni mwa gema kubwa na
kama viongozi wake watakosea kwenye mahesabu yao, wataibadilisha nchi
hiyo na kuwa kambi ya majeshi ya nchi za Magharibi. Ufaransa, Uingereza
na Marekani kwa kuitumia fursa hii iliyopo hivi sasa, zinafanya juhudi
za kulishikia bango suala la mashambulio ya kigaidi ya Boko Haram ili
ziweze kupeleka majeshi yao nchini humo. Makundi kama Boko Haram
yamekuwa yakiundwa na Wamagharibi, kwa lengo la kuzusha ghasia na
machafuko na hatimaye kuichafua taswira ya dini tukufu ya Kiislamu. Hii
ni katika hali ambayo, mashambulio yanayofanywa na kundi la Boko Haram
kwenye misikiti, makanisa na dhidi ya raia wasio na hatia, yako mbali
kabisa na fikra na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Mauaji dhidi
ya watu wasio na hatia kaskazini mwa Nigeria, kidhahiri yanaonekana
kufanyika kwa jina la Uislamu, lakini kiundani ni operesheni na mkakati
maalumu uliopangwa kwenye miaka ya hivi karibuni kwa lengo la
kuuogopesha Uislamu, ili Marekani na washirika wake yaani Uingereza na
Ufaransa waweze kufanikisha malengo yao haramu barani Afrika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment