Kiongozi mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kuna uwezekano
mkubwa kwa Somalia kutumbukia kwenye mgogoro mkubwa wa hali mbaya ya
kibinadamu kutokana na kupungua misaada ya kibinadamu nchini humo.
Philiphe Lazzarini, Mratibu wa masuala ya misaada ya kibinadamu wa Umoja
wa Mataifa nchini Somalia amesema kuwa, upungufu mkubwa wa chakula,
kushadidi maradhi mbalimbali na ukosefu mkubwa wa usalama ni miongoni
mwa mambo yatakayoitumbukiza nchi hiyo kwenye majanga makubwa ya
kibinadamu. Lazzarini ameongeza kuwa, karibu watu milioni mbili na nusu
wanakabiliwa na uhaba wa chakula, lishe duni na maradhi nchini Somalia.
Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, iwapo
hazitachukuliwa hatua za haraka, Somalia itakabiliwa na majanga kama
yale yaliyoikumba nchi hiyo mwaka 2011. Ofisi ya Mratibu wa masuala ya
misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilizitaka nchi wanachama wa
umoja huo kukusanya jumla ya dola milioni 933 kwa minajili ya
kutekelezwa operesheni ya dharura ya kutuma misaada ya kibinadamu nchini
Somalia. Lazzarini amebainisha kuwa, hadi sasa ni kiasi cha dola
milioni 170 tu ndicho kilichokusanywa kutoka kwa nchi wanachama.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment