Hasira za walimwengu zinazoongezeka siku baada ya siku dhidi ya utawala
wa Kizayuni wa Israel zimezidi kuupotezea itibari utawala huo pandikizi
licha ya kupita zaidi ya miongo sita ya kupandikizwa kwake katika kitovu
cha ulimwengu wa Kiislamu na licha ya kutumiwa hila na uayari wa kila
nui wa kuutafutia uhalali utawala huo dhalimu. Hivi sasa utawala wa
Kizayuni unachukiwa zaidi duniani kuliko wakati mwingine wowote huku
walimwengu wakidhihirisha hasira zao kwa utawala huo pandikizi kwa namna
na njia mbalimbali. Wanaharakati wa kupigania amani kutoka nchi
mbalimbali walioko katika Ukanda wa Ghaza wamefanya maandamano kulaani
kuendelea kuzingirwa kidhulma ukanda huo na utawala ghasibu wa Kizayuni.
Waandamanaji hao wamewaenzi wanaharakati 9 wa kupigania amani
waliouliwa katika msafara wa meli wa Marmara uliokuwa unaelekea Ukanda
wa Ghaza kwenda kuvunja mzingiro wa ukanda huo. Mauaji hayo ya kikatili
yalifanywa na makomandoo wa jeshi la Israel mwishoni mwa mwezi Mei 2010.
Mwanaharakati wa amani kutoka Jordan, Kafah al Ma'ayira, ambaye
ameshiriki katika maandamano hayo amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa
Israel haujali kufanya jinai yoyote ile katika njama zake za kujitanua
hata kuua msafara wa watu wasio na silaha uliokuwa unaelekea Ghaza
kwenda kuwasaidia binadamu wengine waliotumbukizwa kwenye mashaka
makubwa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Huko nchini Uhispania pia
kumefanyika harakati ya jamii ya watu wa Vyuo Vikuu, kulaani jinai za
Israel. Malalamiko hayo ya nchini Uhispania yalikuwa sehemu ya kampeni
inayoungwa mkono na zaidi ya wasomi 350 wa Vyuo Vikuu vya nchi hiyo ya
Ulaya wanaosisitiza kuwa taasisi za elimu za utawala wa Kizayuni
zisusiwe na ziwekewe vikwazo kutokana na kushiriki katika kupanua
teknolojia ya utawala huo ambayo inatumiwa kwenye vitendo vya kibaguzi.
Sisitizo la kususiwa na kuwekewa vikwazo taasisi za kielimu za utawala
wa Kizayuni limetolewa pia na vyama vya wanafunzi wa Vyuo Vikuu
mbalimbali nchini Marekani. Miezi michache iliyopita Umoja wa Wanachuo
wa Chuo Kikuu cha Wesleyan nchini Marekani ulipitisha azimio la
kuzisusia taasisi za kielimu za Wazayuni kutokana na taasisi hizo
kushiriki katika uvunjaji wa haki za binadamu katika ardhi za Palestina.
Vyama mbalimbali vya wanachuo wa Vyuo Vikuu vya nchini Uingereza pia
hivi karibuni vilitumia fursa ya mkutano wao wa kumaliza masomo kuwataka
walimwengu waususie utawala wa Kizayuni wa Israel. Ususiaji na vikwazo
vya vituo mbalimbali vya kielimu pamoja na Vyuo Vikuu na magazeti ya
kona mbalimbali duniani dhidi ya utawala wa Kizayuni vimepata nguvu sana
mwaka huu wa 2014. Matukio ya kimataifa yanaonesha kuwa, kutengwa
utawala wa Kizayuni kimataifa hakuishii tu katika masuala ya kisiasa,
kiuchimi na kidiplomasia, bali kutengwa Israel katika masuala ya
kiutamaduni na Vyuo Vikuu nako kumeongezeka sana hivi sasa kuliko wakati
mwingine wowote. Jinai za utawala wa Kizayuni kwa wananchi wa Palestina
zimezijeruhi vibaya nyoyo za walimwengu na jinai hizo ndizo
zinazoongeza hasira za walimwengu dhidi ya Israel. Vile vile kuendelea
siasa za utawala wa Kizayuni za kupora na kukalia kwa mabavu ardhi za
Wapalestina na za mataifa mengine na kutokana na utawala huo kukaidi
sheria zote za kimataifa kumezifanya nchi nyingi za dunia zikiwemo hata
za barani Ulaya kushindwa kuvumilia na hivyo kuamua kuulalamikia utawala
wa Kizayuni na kuchukua hatua za kivitendo vya kuwaunga mkono wananchi
wanaodhulumiwa wa Palestina na hususan wa Ukanda wa Ghaza, kwa lengo la
kuwaondolea wakazi wa ukanda huo, mzingiro waliowekewa kila upande na
Wazayuni kwa miaka kadhaa sasa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment