Jumuiya mbalimbali kama vile Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, ECOWAS
pamoja na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamelaani
ghasia na machafuko ya hivi karibuni katika eneo la Kidal, kaskazini mwa
Mali. Taarifa ya jumuiya hizo imesema mapigano yaliyoripotiwa hivi
karibuni kati ya vikosi vya serikali ya Mali na wapiganaji wa makundi ya
waasi ni ukiukaji wa makubaliano ya amani yaliyosainiwa na pande mbili
hizo nchini Burkina Faso mwezi Machi mwaka uliopita. Jumuiya hizo
zimesisitiza udharura wa kufanyika mazungumzo ya haraka kati ya pande
hasimu ili hali ya utulivu irejee mara moja.
Siku ya Jumamosi kulitokea makabiliano makali kati ya waasi na jeshi
la serikali katika eneo la Kidal ambapo watu kadhaa waliuawa na wengine
kujeruhiwa. Mapigano hayo yalitokea wakati Waziri Mkuu wa Mali, Musi
Mara alipokuwa ziarani katika eneo hilo la Kidal. Baadhi ya duru
zinasema waasi wamewateka nyara watu 30 wakati wa patashika hiyo.
Wapinzani wa serikali wanaojumuisha kundi la Tuareg na lile la Ansaru
Din wanapigania kujitenga eneo la kskazini mwa Mali.
No comments:
Post a Comment