Mapigano makali yanaendelea kushuhudiwa nchini Libya huku wanamgambo
watiifu kwa Khalifa Haftar, jenerali mstaafu na kamanda wa zamani wa
jeshi la nchi kavu nchini humo wakisonga mbele hadi Tripoli, mji mkuu wa
Libya. Mashambulio ya makombora na mizinga ya wanamgambo wanaobeba
silaha kwenye makao ya Kongresi ya Taifa ya Libya yaani bunge
yanaonyesha kuwa, Libya imetumbukia kwenye lindi la ukosevu wa amani.
Duru za kisiasa zinasema kuwa, kile kinachojitokeza nchini Libya ni
mithili ya mapinduzi.
Kongresi ya Taifa ya Libya, chombo pekee cha
kutunga sheria nchini humo imesimamisha shughuli zake na hii ni katika
hali ambayo wanamgambo pia wameshambulia majengo ya televisheni mjini
Tripoli. Mapigano kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo watiifu kwa
Jenerali mstaafu Khalifa Haftar yangali bado yanaendelea mjini Tripoli.
Salah al Marghani Waziri wa Sheria wa Libya ametangaza kuwa, karibu watu
60 wameuawa na kujeruhiwa kwenye mapigano yaliyotokea jana mjini
Tripoli. Duru za habari zinasema kuwa, maeneo ya kiistratijia ya Libya
yamekuwa yakilengwa na mashambulizi ya wanamgambo hao. Dalili zote
zinaonyesha kwamba wanamgambo wanafanya juhudi za kutaka kupora madaraka
kwa nguvu nchini humo. Swali linalojitokeza hapa ni hili kwamba, je
senario ya Misri inaweza kukaririwa nchini Libya? Nchini Libya,
wanajeshi waliopata mafunzo ya kijeshi wakati wa utawala wa Kanali
Muammar Gaddafi, hivi sasa ndio wanaoendesha harakati za kijeshi dhidi
ya serikali ya mpito na hata kufika Tripoli wakitokea mji wa Benghazi
ulioko mashariki mwa nchi hiyo. Hatua ya wanamgambo hao ya kulilazimisha
bunge kufunga shughuli zake, ni mwanzo wa kutatiza shughuli za
uendeshaji wa serikali ya Libya. Inaonekana kuwa, wanajeshi wa zamani
wanataka kuzusha ghasia na machafuko ili waweze kufikia malengo yao.
Jenerali mstaafu Khalifa Haftar na wanamgambo watiifu kwake wanaelewa
vyema kwamba, Libya haina jeshi imara na lenye nguvu. Hivi sasa nchi
hiyo imegawanyika katika makundi mbalimbali yakiwemo ya wanamgambo,
wanamapinduzi wa zamani na makumi ya makundi mengine ya kisiasa,
kikabila na ya kijeshi na kila kundi limejizatiti na kudhibiti baadhi ya
maeneo nchini humo. Sababu hiyohiyo ndiyo iliyopelekea Jenerali mstaafu
Haftar na wafuasi wake watiifu kutunisha misuli yao dhidi ya majeshi ya
serikali. Hali inayotawala hivi sasa nchini Libya inaonyesha kuwa,
kundi lolote litakaloweza kutoa pigo dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo
linatarajiwa kushika hatamu za uongozi katika siku zijazo. Imeelezwa
kuwa Jenerali huyo mstaafu amekuwa na nguvu zaidi za kijeshi kutokana na
uwezo wake wa kuzidhibiti kambi zote za kijeshi na kiusalama katika
eneo lenye utajiri mkubwa wa mafuta lililoko mashariki mwa nchi hiyo.
Jenerali mstaafu Haftar anafanya juhudi za kushambulia maeneo muhimu na
nyeti, ili aweze kuidhoofisha serikali na hatimaye kuchukua hatamu za
uongozi. Baadhi ya duru za kisiasa zinaamini kwamba, wanajeshi wastaafu
wa utawala wa Gaddafi wanapanga mikakati ya kurejea kwenye uwanja wa
kisiasa nchini humo. Iwapo hali hiyo itathibiti, bila shaka hali ya
kisiasa ya Libya itafanana na ile ya Misri, na bila shaka nchi za
Magharibi ndizo zitakazonufaika na hali hiyo. Uzoefu unaonyesha kuwa,
nchi za Magharibi zinaweza kuwa bega kwa bega na wanajeshi.
Inavyoonekana ni kuwa, hali inayoshuhudiwa hivi sasa katika nchi za
Misri na Libya, ni kwa wanajeshi kuwa katika mikakati ya kuchukua
madaraka. Kwa vile Libya inakabiliwa na machafuko kama ilivyokuwa
Misri, hakuna shaka kuwa nchi hiyo kwa mara nyingine tena itakabiliwa na
hatima ya kuingiliwa na Marekani na madola ya Magharibi katika harakati
za kisiasa za nchi hiyo. Bila shaka nchi hizo zinaingilia mambo ya
ndani ya nchi nyingine kwa lengo la kudhamini maslahi yao haramu barani
Afrika, kwa kupora maliasili na utajiri wa mafuta. Hivi karibuni, Rais
Barack Obama wa Marekani alitahadharisha kwamba, iwapo Libya itashindwa
kurejesha amani na utulivu, nchi hiyo pamoja na wanachama wengine wa
NATO wataingilia mgogoro wa nchi hiyo iliyoko kaskazini mwa Afrika kwa
lengo la kuongoza mwenendo wa kisiasa wa nchi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment