Matokeo ya awali ya kura za urais zilizopigwa na
Wamisri waishio nje ya nchi yanaonyesha wazi kwamba, jeshi la nchi hiyo
karibuni hivi litachukua tena madaraka katika nchi hiyo ya kaskazini mwa
Afrika. Duru zinaripoti kwamba, mkuu wa zamani wa jeshi Abdul-Fattah
al-Sisi amepata takriban asilimia 90 ya kura zilizohesabiwa za Wamisri
waishio nje ya nchi. Ingawa matokeo hayo hayajatangazwa rasmi lakini
wapembuzi wa mambo wanasema mipango ya nyuma ya pazia inaendelea
kupangwa kati ya al-Sisi na viongozi wa sasa katika serikali ya mpito ya
nchi hiyo.
Weledi wa mambo wanaamini kwamba al-Sisi mwisho wa siku
ataibuka na ushindi na anachosubiri kwa sasa ni uchaguzi mkuu wa rais
kwa Wamisri walioko nyumbani. Zoezi hilo linatarajiwa kufanyika Mei 26
na 27 yaani baadaye wiki ijayo.
Wafuatiliaji wa siasa za Misri wanasema uchaguzi huo ni wa
kimaonyesho tu kwani mahesabu yake yalipangwa na kuratibiwa kitambo na
kwamba matokeo yake tayari yashajulikana hata kabla ya upigaji kura
ndani ya Misri kuanza. Wachanganuzi hao wanasema kuweko wagombea wawili
tu wa urais kwenye uchaguzi wa Misri ambapo mmoja wao ni mwanajeshi wa
zamani ni ishara tosha kwamba jeshi linajiandaa kurudi tena madarakani
baada ya kamanda wao mkuu, Hosni Mubarak kuangushwa na wananchi mwaka
2011.
Jenerali Abdul-Fattah al-Sisi ambaye anapigiwa upatu
kushinda kwenye uchaguzi huo amekuwa akisema lengo lake la kugombea
urais ni kutaka kukabiliana na umasikizi, kurejesha usalama ndani ya
Misri pamoja na kuimarisha uchumi unaoyumba wa nchi hiyo. Mapendekezo
kama hayo pia yametolewa na mgombea wa pili wa urais wa Misri, Hamdeen
Sabahi ambaye wadadisi wengi wa kisiasa wanasema amewekwa na jeshi
kwenye kinyang'anyiro hicho ili kuonyesha kuna ushindani na demokrasia
nchini.
Hapana shaka kuwa, jeshi limekuwa na satua kubwa katika
siasa za Misri kwa muda mrefu na baada ya kuangushwa utawala wa dikteta
Hosni Mubarak mwaka 2011, jeshi hilo lililazimika kujifungia faraghani
na kuandaa mikakati mipya ya kurudi tena katika safu za juu za uongozi
wa taifa hilo. Weledi wa mambo wanasema rais aliyepinduliwa Dkt.
Mohammad Morsi alishindwa kuimarisha uchumi kutokana na hujuma za wazi
za maafisa wa jeshi. Hujuma hizo zilikuwa sehemu ya mpango wa kufelisha
utawala wa Dkt Morsi ili wananchi waliokuwa na matumaini makubwa kwake
waanze kumpinga na kisha kumuondoa madarakani. Kwa kiwango fulani, jeshi
lilifanikiwa kufikia lengo hilo.
Yote hayo yakiwa tisa, kumi ni kwamba, kurudi tena jeshi la
Misri katika medani ya siasa za nchi hiyo kumetokana na ridhaa ya
Wamagharibi wakiongozwa na Marekani. Daima nchi za Magharibi zimekuwa
zikitaka jeshi liendelee kutawala huko Misri ili kulinda maslahi ya
utawala haramu wa Israe na ndio maana hata baada ya jeshi kumpindua rais
aliyechaguliwa kihalali na wananchi, Mohammad Morsi, nchi hizo
hazikulaani moja kwa moja mapinduzi hayo. Ili kujitoa kimasomaso zilitoa
vitisho visivyotekelezeka dhidi ya majenerali lakini nyuma ya pazia
ziliendelea kuunga mkono harakati za jeshi za kurejea tena madarakani
katika sura inayoonekana kuwa ya kidemokrasia.
No comments:
Post a Comment