Harakati ya Baraza Kuu kwa
Ajili ya Umoja wa Azawad (HCUA) imetangaza kuwa iko tayari kufanya
mazungumzo na viongozi wa serikali ya Mali. Harakati hiyo aidha imesema
iko tayari kuitambua rasmi bendera ya taifa na kuheshimu makubaliano ya
amani yaliyotiwa saini tarehe 18 Juni mwaka jana nchini Burkina Faso.
Wataalamu wa mambo wana matumaini kwamba misimamo hiyo iliyoonyeshwa na
harakati ya Baraza Kuu kwa Ajili ya Umoja wa Azawad itaandaa mazingira
ya kurejea kwa kiwango fulani amani na uthabiti nchini Mali.
Kabla ya
hapo kusainiwa makubaliano ya amani na kufanyika uchaguzi wa rais na
bunge havikuweza kusaidia kuleta utulivu na uthabiti wa kudumu huko
kaskazini mwa nchi hiyo. Harakati ya HCUA ni moja ya makundi ya Watuareg
yanayobeba silaha. Harakati hiyo imeitaka Jamii ya Kimataifa ipendekeze
mpatanishi na kuitisha mazungumzo katika nchi isiyopendelea upande
wowote. Harakati ya Umoja wa Azawad aidha imetangaza kwamba baada ya
kufanyika mazungumzo itahakikisha harakati na makundi mengine yote
yanayojulikana kuwa ni wapinzani wa serikali ya Mali yanaunganishwa na
harakati hiyo. Itakumbukwa kuwa huko nyuma wawakilishi wa makundi
yanayobeba silaha ya Watuareg likiwemo hilo la Baraza Kuu kwa Ajili ya
Umoja wa Azawad, harakati ya Taifa ya Ukombozi wa Azawad (MNLA),
harakati ya Waarabu wa Azawad (MAA) pamoja na makundi mengine mawili ya
vikosi vya watani na vya muqawama yalisaini hati ya maelewano na kuahidi
kukomesha utumiaji nguvu na mabavu kama njia ya kubainisha maoni na
mitazamo yao. Wawakilishi wa makundi yote hayo walisisitiza pia juu ya
hamu yao ya kuona amani inarejea nchini Mali.Viongozi wa serikali ya Bamako wamekaribisha wazo la kufanyika mazungumzo na kueleza kwamba mtazamo wa utumiaji mabavu unakwamisha maendeleo ya eneo zima. Waziri Mkuu wa Mali Moussa Mara ametilia mkazo juu ya kufikiwa maridhiano ya kitaifa kati ya serikali na makundi ya upinzani yanayobeba silaha na kupatikana mwafaka wa kisiasa ili kuhitimisha mgogoro wa kaskazini mwa nchi hiyo. Wakati huohuo kuna ripoti kwamba mazungumzo yamefanyika kati ya makundi yanayobeba silaha nchini Mali na maafisa wa serikali ya Algeria ili kuandaa utangulizi wa mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa nchini Mali. Katika upande mwengine baadhi ya wakosoaji wanamtuhumu Rais Aboubakr Keita wa Mali kwa kupoteza fursa ya kuutatua kwa njia ya amani mgogoro wa nchi hiyo. Kwa mtazamo wa wakosoaji hao, Keita hakuheshimu makubaliano ya usitishaji vita na makundi ya upinzani. Wachambuzi wa mambo wana matumaini kuwa mabadiliko ya baraza la mawaziri yaliyofanyika tarehe 5 Aprili na kuteuliwa Moussa Mara kuwa Waziri Mkuu mpya vitafungua njia ya kuhimitisha harakati za wanamgambo wa Kituareg huko kaskazini mwa Mali. Kabla ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Machi 2012 Mali ilikuwa moja ya nchi zenye demokrasia yenye uthabiti mkubwa zaidi katika eneo la magharibi mwa Afrika. Lakini kukosekana kwa serikali yenye nguvu kulifungua njia kwa makundi ya upinzani yanayobeba silaha kushika hatamu za utawala wa nchi hiyo
No comments:
Post a Comment