Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ametangaza habari ya
kugunduliwa njama ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli nchini
humo. Kiir ametangaza kuwa vikosi vya usalama vya Sudan Kusini
vimefanikiwa kugundua na kuzima njama za jaribio hilo la mapinduzi ya
kijeshi dhidi ya serikali yake. Katika hali ambayo hakuna taarifa za
uhakika na kamili zilizopatikana hadi sasa kuhusu njama za jaribio hilo
la mapinduzi, weledi wa mambo wanaamini kuwa kitendo hicho kimetekelezwa
katika muendeleo wa mashindano ya kuwania madaraka huko Sudan Kusini.
Rais Salva Kiir Mayardit amesisitiza kuwa Rick Machar Makamu wake wa
zamani ni miongoni mwa watu waliotiwa mbaroni kwa tuhuma za kupanga
jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi. Rick Machar ambaye alifukuzwa kazi
tarehe 25 mwezi Julai kwa amri ya Rais wa Sudan Kusini, alikuwa tayari
ametangaza nia yake ya kuwa mgombea katika uchaguzi wa rais uliopangwa
kufanyika nchini humo mwakani, kabla ya hata ya kuuzuliwa. Weledi wa
masuala ya kisiasa wanasema kuwa Rick Machar ameuzuliwa uongozi ili
kufuta upinzani wa shakhsiya huyo kwa Salva Kiir Mayardit katika
uchaguzi ujao. Baadhi ya duru za habari zilionyesha kutiwa shaka na
hatua ya kufutwa kazi Makamu wa Rais Rick Machar na mawaziri wengine
wawili wa serikali ya Sudan Kusini na kuhoji kama ilikuwa ni ya
kulifanyia marekebisho baraza la mawaziri au kuanza mgogoro wa kisiasa
nchini humo. Kwa mtazamo huo, vita vya kuwania madaraka kati ya
mwanasiasa Rick Machar na Rais Salva Kiir Mayardit, vinaonekana kuwa na
historia ya tangu huko nyuma. Vita vya kuwania madaraka kati ya mahasimu
hao wawili wa zamani huwenda vikaisababishia mgogoro wa muda mrefu
Sudan Kusini nchi iliyoasisiwa hivi karibuni.
Sudan Kusini ilitangazwa kuasisiwa na kuwa nchi huru tarehe
9 mwezi Julai mwaka 2011. Weledi wa mambo wanaamini kuwa kujitenga
Sudan Kusini na Sudan ni matokeo ya ushawishi wa Marekani na utawala wa
Kizayuni pande ambazo zilifanya kila zilichoweza kuigawa vipande Sudan
lengo likiwa ni kudhamini maslahi haramu ya Washington na utawala
unaopenda kujitanua wa Tel Aviv. Hasa ikizingatiwa kwamba utajiri mkubwa
wa maliasili ya mafuta ya Sudan upo Sudan Kusini na nchi hiyo inahitaji
taasisi za mafuta zilizoko Sudan kwa ajili tu ya kuchimba na kupitishia
mafuta ghafi yake. Utawala ghasibu wa Israel daima umekuwa ukitoa
zingatio maalumu kwa bara la Afrika na maeneo yake ya kiistratejia. Nchi
kama Uganda, Kenya na Ethiopia ni miongoni mwa waitifaki wa Israel
katika eneo la Mashariki mwa Afrika zenye nafasi muhimu katika siasa za
nje za utawala wa Kizayuni. Katika mgawanyo wa kijiografia wa bara la
Afrika, eneo linalozijumuisha Sudan, Kenya, Uganda na Tanzania pamoja na
nchi nne za eneo la Pembe ya Afrika, zinajulikana kwa jina la"Afrika
Mashariki Kubwa." Eneo hilo pia limekuwa na nafasi makhsusi katika siasa
za nje za Marekani. Hii ni kwa sababu Afrika Mashariki Kubwa kwa kuwa
na Ghuba ya Aden, bahari Nyekundu na ya Hindi linatambuliwa kuwa mhimili
mkuu wa njia za kimataifa za biashara ya mafuta. Kwa hiyo si jambo
lililo mbali kwamba mkono wa Marekani na utawala wa Kizayuni ukawa uko
nyuma ya pazia la matukio ya ndani yanayojiri hivi sasa huko Sudan
Kusini.
No comments:
Post a Comment