Dar es Salaam. Biashara ya dawa za kulevya
nchini inazidi kuchukua sura mpya ambapo sasa wanawake wanaouza vyakula,
maarufu mama ntilie, hutumika kusambaza dawa hizo kwa wateja.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa muda mrefu
katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam unaonyesha kuwa biashara
hiyo inafanyika katika maeneo ya Tandika, Manzese, Vingunguti, Temeke,
Tandale, Mtongani na Keko.
Wanawake hao wamekuwa wakitumia mwanya wa kuuza
chakula kama kinga yao, huku biashara yao kubwa ikiwa ni kuuza dawa za
kulevya aina ya heroin, bangi na aina nyingine.
Mbinu hii mpya ya usambazaji wa dawa za kulevya
kwa kutumia wanawake wanaouza vyakula imeelezwa kuwa inawasaidia
wahusika wakuu, kuendesha biashara yao kwa ufanisi zaidi.
Uchunguzi umeonyesha kuwa wafanyabiashara wa dawa
hizo wameamua kuwatumia mamalishe kutokana na kuwa waaminifu na
kuhudumia wateja wengi, hivyo ni vigumu watu kuwashtukia wakiwamo askari
polisi.
Imebainika kuwa dawa hizo huuzwa kulingana na
maeneo, wakati maeneo ya watu wasiokuwa wa uwezo hupimwa kwa kutumia
kipimo kidogo zaidi kwa bei ya chini ambayo watumiaji husika huweza
kuimudu.
Aidha dawa hizo hufungwa katika mitindo miwili
tofauti, ukiwa katika unga wa vidonge na wa kawaida ingawa bei zake
hazitofautiani sana.
Uchunguzi unaonyesha kuwa vidoge huuzwa vikiwa vizima au vipande, huku unga wa kawaida ukiuzwa kwa kipimo maalumu.
Kwa kawaida ‘unga’ huo huuzwa kwa Sh1,000 kwa
pointi huku kete moja ikiuzwa kwa Sh2,000, wakati vidonge, kizima huuzwa
kwa Sh2,000, huku kipande huuzwa kwa Sh1,000 zikitofautiana kulingana
na maeneo.
Dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Asha
(28) ambaye siyo jina lake halisi ni muuzaji mkubwa wa dawa hizo. Awali
alikuwa akifanya shughuli zake hizo za uuzaji katika maeneo ya Yombo
Kilakala, ingawaje hivi sasa amehamia Temeke.
“Unajua siku zote dhumuni la kufanya biashara ni
kupata faida, hivyo naweza kusema niliingia kwenye biashara hii kwa
sababu tu ina faida zaidi kuliko biashara nyingine,” anasema.
Awali alikuwa akiuza vyakula huku akifanya biashara hiyo ya
kuuza dawa, baadaye akaacha kuuza vyakula akabaki na biashara ya dawa za
kulevya.
Akielezea namna anavyofanya biashara yake hiyo,
Asha anasema kwa kawaida huwa ananunua mkanda ambao unakuwa umefungwa
vidoge vidogovidogo kumi hadi ishirini. Mara nyingi huuza kulingana na
mahitaji ya mteja.
“Halafu baada ya kununua hivyo huwa nauza kidogokidogo vidonge hivyo.
Kwa kawaida kidoge kimoja huwa nauza kati ya
sh1,000 hadi Sh2,000. Bei yake hutegemea na mahali unapouzia. Kama
unauzia watu waliochoka sana inabidi upaki kidogokidogo ili kuweza
kuliteka soko lao,” anasema.
“Nimefanya biashara hii kwa muda wa miaka mitatu,
lakini ukweli ni kwamba hadi sasa nimefanikiwa kwa kiasi fulani.
Nimeweza kujenga nyumba ya kwangu mwenyewe, pia kuhudumia familia yangu.
Licha ya kuwa na madhara kwa watu, lakini ukweli ni kuwa biashara ya
unga inalipa,” anasisitiza.
Abubakari Ismail (33) aliyewahi kutumia dawa za
kulevya, ambaye kwa sasa ni kiongozi wa kupambana na dawa hizo
kinachofahamika kama Use Ant -Drugs, kilichopo Yombo, wilayani Temeke,
anasema kuwa tatizo la wanawake kujihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya
linachangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha mapambano dhidi ya dawa hizo
hususan kwa vijana.
‘Joseph (17)’, siyo jina lake halisi ni kijana
aliyekuwa katika matibabu kutokana na matumizi ya dawa za kulevya. Hivi
sasa kijana huyu amelazimika kuhama nyumbani kwao kutokana na kumkimbia
mama yake mzazi ambaye anajihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya.
Mkurugenzi wa Kituo cha Makangarawe Youth
Information Center cha jijini Dar es Salaam, kinachojishughulisha na
miradi kadhaa ya vijana ikiwamo mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa
vijana, Ismail Mnikite, amesema kitendo cha wanawake kushiriki katika
uuzaji wa dawa za kulevya ni tatizo jipya linalochangia kukwamisha
juhudi za mapambano hayo.
No comments:
Post a Comment