Kanali wa zamani katika Jeshi la Rwanda ambaye alikuwa akisakwa kwa
kuhusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini humo ametiwa
mbaroni nchini Ufaransa.
Imearifiwa kuwa Kanali Laurent Serubuga alitiwa mbaroni Alkhamisi
karibu na mji wa Cambrai kaskazini mwa Ufaransa. Wakili wake, Thierry
Massis amesema Serubuga mwenye umri wa miaka 75 atafikishwa mahakamani
Alkhamisi ijayo.
Imearifiwa kuwa katika mauaji ya kimbari ya Rwanda
yaliyojiri kati ya Aprili na Julai mwaka 1994, Serubuga alikuwa naibu
mkuu wa jeshi. Katika kipindi hicho watu zaidi ya laki nane waliuawa
wakati watu wa Kabila la Hutu walipochochewa kutekeleza mauaji dhidi ya
Watutsi.
Alain Gauthier mkuu wa kundi la waathirika wa mauaji ya kimbari
Rwanda CPCR amesema kutiwa mbaroni Serubuga ni 'habari nzuri'. Ameongeza
kuwa kanali Serubuga anapaswa kubeba lawama sawa na kanali Theoneste
Bagosora. Itakumbukwa kuwa mwaka 2011 Mahakama ya Kimatiafa ya Jinai za
Rwanda ilimtaja Bagosora kuwa mratibu mkuu wa mauaji ya kimbari ya
Rwanda na kumhukumu kifungo cha miaka 35 gerezani. Serikali ya Rwanda
kwa mara kadhaa imewatuhumu maafisa wa ngazi za juu wa Ufaransa kuwa
walihusika katika mauaji hayo ya kimbari.
No comments:
Post a Comment