Serikali ya Marekani inapanga kuwasiliana na rais-mteule wa Iran na
kumjulisha azma ya Washington ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana
kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu.
Press TV imenukulu ripoti ya gazeti la Marekani la The Wall Street
Journal ambalo limeandika kuwa, maafisa wa Marekani Jumanne ijayo
wanakutana na wawakilishi wa nchi zingine nne wanachama wa Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa ili kujadili njia za kuamiliana na
rais-mteule wa Iran kuhusu kadhia ya nyuklia.
Iran imekuwa ikifanya mazungumzo na kundi la 5+1 ambalo
linazikutanisha pamoja Marekani, Uingereza, Ufaransa, Uchina na Russia
pamoja na Ujerumani. Mazungumzo hayo yamehusu masuala kadhaa huku kadhia
muhimu zaidi ikiwa ni miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani.
Mkuu wa Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya Catherine Ashton Ijumaa
ya jana alisema kundi la 5+1 linataka hatua imara zichukuliwe katika
mazungumzo na Iran.
Marekani, Israel na baadhi ya waitifaki wao wamekuwa wakiituhumu Iran
kuwa ina malengo ya kijeshi katika miradi yake ya kuzalisha nishati ya
nyuklia. Iran imekanusha madai hayo na kusema shughuli zake za nyuklia
zinafanyika kwa malengo ya amani katika fremu ya sheria za kimataifa na
chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.
No comments:
Post a Comment