Siku tatu baada ya
Rais Jakaya Kikwete kuponda mpango wa Chadema kuanzisha kambi kwa ajili
ya mafunzo ya ulinzi kuwalinda viongozi na wanachama wake, chama hicho
kikuu cha upinzani nchini kimeibuka na kusema kuwa kinaendelea na
mpango huo na kambi hizo zitaanza rasmi wiki ijayo.
Kimesema hakitishwi na kauli ya Jeshi la Polisi
kukionya juu ya uanzishwaji wa mafunzo hayo, kwamba jeshi hilo
linatakiwa kuanza kukizuia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwanza, kwa
maelezo kuwa chama hicho tawala pia kina kikundi cha ulinzi ‘Green
Guards’ ambacho kinafanya mafunzo ya kijeshi, huku kikitumia silaha za
moto.
“CCM ndiyo wataipeleka nchi hii pabaya,
wanawafundisha vijana huku wakiwabebesha bunduki, wanajenga taifa la
aina gani, bunduki ni silaha ya kivita sasa wanaandaa watu kupigana na
nani” alisema Mkurugenzi wa Organaizesheni na Mafunzo wa chama hicho,
Benson Kigaira jana wakati akizungumza na wanahabari huku akionyesha
picha za mafunzo ya CCM, zinazoonyesha vijana wakiwa wamebeba silaha
(hata hivyo ni mbao zilizotengenezwa kwa mfano wa bunduki).
Wakati Chadema wakieleza hayo, CCM kimeshtushwa na taarifa hizo na kueleza kuwa hali hiyo sasa inahatarisha usalama wa nchi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho
(UVCCM), Martin Shigela alisema ni vyema Chadema kikawaambia wananchi
wawalinde, kuliko kuanzisha mafunzo huku akimtaka Msajili wa Vyama vya
siasa nchini, John Tendwa kulitizama kwa kina suala hilo.
Akifunga Kongamano la Amani lililoandaliwa na
Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Dar es Salaam Julai 10, mwaka huu,
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa pia alikosoa kitendo
cha Chadema kususia kongamano hilo alisema, “Sasa hawa kweli wanapenda
amani yetu wakati hawapendi tuzungumze wanataka watu wauane, wapigane.”
Mbali na Rais Kikwete, Msemaji wa Jeshi la Polisi
nchini, SSP Advera Senso juzi alikionya chama hicho kuhusu mpango huo
akisema kuwa kitendo cha chama chochote cha siasa kikiwemo Chadema,
kuanzisha kikundi cha kujihami ni kinyume na sheria za nchi na endapo
watafanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kauli ya jana ya Chadema ni mwendelezo wa ile
iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe Julai 9, mwaka
huu, ambapo alisema kimechukua hatua hiyo baada ya Serikali na vyombo
vyake vya ulinzi na usalama kushindwa kufanyia kazi malalamiko yao
kuhusu mauaji, vitisho na matukio ya kutisha wanayofanyiwa baadhi ya
viongozi na wanachama wao.
Katika ufafanuzi wake Kigaila alisema Chadema
hakianzishi vikundi vya kijeshi, bali mafunzo ya kuwafundisha walinzi
wa chama hicho ‘Red Brigade’, jinsi ya kujilinda.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni haki kwa raia yeyote kujilinda, Chadema ni taasisi ni haki
yetu kuilinda taasisi yetu ndiyo maana tumesajili kikundi chetu cha
ulinzi, sasa nani anatutisha, tunataka polisi waanze na CCM kwanza ambao
katika mafunzo yao wanafundisha hadi kupiga saluti na kutumia silaha,”
alisema.
Alisema mafunzo hayo yataanza rasmi wiki ijayo,
huku akisita kutaja siku yatakayoanza, wala mikoa yatakayofanyika na
kusisitiza kuwa hayo yatatangazwa wiki ijayo wakati vijana wakienda
katika mafunzo.
Tuhuma
Alisema kabla ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga
mwaka 2011, CCM kilianzisha kambi ya vijana eneo la Ulemo wilayani
Iramba katika Jimbo la Iramba Magharibi na kwamba kambi hiyo ilikuwa
na vijana 200.
Alifafanua kwamba katika uchaguzi mdogo wa Jimbo
la Igunga CCM ilianzisha kambi katika wilayani Nzega, Tabora,
Shinyanga na Singida Mjini za kambi hizo zilikuwa na vijana 800.
“Vijana hao walipelekwa katika uchaguzi wa Igunga
na kusababisha kifo cha kada wa Chadema, Msafiri Mbwambo ambaye alikuwa
wakala wa chama katika uchaguzi huo, awali tuliwaeleza polisi jinsi
kambi hizo zilivyowekwa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka leo,”
alisema.
Alisema mwaka jana CCM ilifanya mafunzo ya kitaifa
ya vijana wao wa ‘Green Guards’ mkoani Mwanza na baada ya mafunzo hayo
walifanya gwaride la kijeshi.
Alisema wakati vijana hao wakihitimisha mafunzo
hayo walikaguliwa na Mwenyiki wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete,
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Phillip Mangula pamoja na Katibu
Mkuu, Abdulrahman Kinana, huku wakipigiwa saluti na vijana hao waliokuwa
wamebeba ‘matoi’ yaliyotengenezwa kwa mfano wa bunduki.
“CCM wanasema kuwa Green Guards wanafundishwa
ujasiriamali, hivi watu wanaofundishwa ujasiriamali huwa wanapigiana
saluti, huwa wanabeba ‘matoi’ yenye mfano wa bunduki,” alihoji.
Alisema kambi za CCM zilianza tangu mwaka 2007
wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiteto, na kufafanua kuwa katika
uchaguzi huo baadhi ya viongozi wa Chadema akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa
chama hicho Zanzibar, Hamad Musa Yusuf walipigwa na Green Guards huku
polisi wakishuhudia.
Kauli ya CCM
Uanzishwaji wa mafunzo hayo umeonekana wazi
kukitesa CCM ambapo jana Shigela alisema “Chadema kabla ya kuanza kutoa
mafunzo hayo kwa vijana hao (Red Brigade) wanatakiwa kuwaeleza wananchi
dhamira halisi ya kuanzishwa kwake, kama siyo kuchochea uvunjifu wa
amani.”
“Chadema ni chama cha siasa, kinaomba kuwatumikia
wananchi wanaowapigia kura wenyewe hivyo kama wanaona hawatendewi haki
na polisi wawaambie wananchi wenyewe wawalinde lakini si kuanzisha,
kutoa mafunzo hayo kwa vijana.”
No comments:
Post a Comment