Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Wednesday, July 10, 2013

Mawaziri wa SADC kukutana kesho DAR

Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Ustawi ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), wanatarajiwa kukutana kuanzia kesho hadi Julai 13 nchini Tanzania. Mawaziri hao wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ikiwemo hali ya kisiasa kusini mwa Afrika, uimarishaji wa demokrasia, Utekelezaji wa Mpango na Mkakati wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC, mikataba ya ushirikiano katika nyanja za Ulinzi na Usalama pamoja na ushirikiano baina ya SADC na Umoja wa Ulaya (EU).
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania, imesema kuwa, kikao hicho kitatanguliwa na cha makatibu wakuu na maofisa waandamizi kitakachofanyika Julai 10 na 11 ambacho kitahudhuriwa na nchi zote wanachama wa SADC isipokuwa Madagascar, ambayo imesimamishwa uanachama katika jumuiya hiyo. Taarifa hiyo imebainisha kwamba, mawaziri hao watakutana Julai 13, chini ya uenyekiti wa Bernard Membe Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania.

No comments: