Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR)
limetangaza kuwa, maelfu ya Wakongomani wamekimbilia katika nchi jirani
ya Uganda kufuatia machafuko yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, zaidi
ya raia elfu thelathini wamekimbia makazi yao mashariki mwa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo na kuingia nchini Uganda.
Taarifa zaidi zinasema
kuwa, wakimbizi hao kwa sasa wamepatiwa hifadhi katika eneo la
Bundibugyo magharibi mwa Uganda.
Wakati huo huo, hali katika jimbo la Kivu Kaskazini inaripotiwa
kuanza kurejea katika hali ya kawaida baada ya jeshi kudhibiti jimbo
hilo jana usiku. Katika upande mwingine, jeshi la Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo limefanikiwa kuyadhibiti maeneo ya mpaka wake na
Uganda. Majeshi ya Congo yamewasili katika maeneo hayo na kufanikiwa
kuwafurusha wapiganaji wa kundi la waasi la ADF-NALU linalopigana dhidi
ya serikali ya Kampala.
No comments:
Post a Comment