Hii leo makundi ya upinzani nchini Ethiopia yameitisha maandamano
makubwa dhidi ya serikali ya nchi hiyo. Kufanyiwa marekebisho sheria na
uhuru wa raia, kuheshimiwa katiba na kutekelezwa usawa wa kijamii, ni
miongoni mwa matakwa ya wapinzani hao. Inasemekana kuwa, sambamba na
polisi kutoa onyo dhidi ya wapinzani, imechukua pia hatua kali za
kiusalama kwa ajili ya kukabiliana na maandamano hayo.
Uingiliaji wa
muda mrefu ndani ya masuala ya kidini unaofanywa na serikali ya Addis
Ababa, umeibua hasira za wafuasi wengi wa dini mbalimbali nchini humo.
Itakumbukwa kuwa, Ijumaa iliyopita maelfu ya Waislamu nchini humo
waliandamana kulalamikia hatua ya serikali ya kuingilia mambo yao.
Maandamano hayo yalienda sambamba na kumbukumbu ya kutiwa mbaroni na
maafisa usalama wa Ethiopia, makumi ya Waislamu na viongozi wao nchini
humo. Itakumbukwa kuwa, tarehe 12 Julai mwaka jana maafisa usalama wa
nchi hiyo, walivamia msikiti wa An-war ambao ndio msikiti mkubwa zaidi
mjini Addis Ababa na kuwatia mbaroni idadi kubwa ya Waislamu wakiwemo
masheikh. Hii ni katika hali ambayo, hadi sasa Waislamu hao bado
wanaendelea kuteseka katika korokoro za vyombo vya usalama vya Ethiopia.
Serikali ya Ethiopia inadai kwamba, Waislamu 74 waliotiwa mbaroni Julai
12 mwaka jana walitenda kosa la uchocheaji wa vurugu. Waislamu nchini
humo wanaunda karibu asilimia 34 ya jamii ya raia milioni 85 ya nchi
hiyo. Kimsingi ni kuwa, katiba ya nchi hiyo ni ya kisekula isiyoheshimu
dini, hata hivyo viongozi wa serikali ya Addis Ababa wamekuwa wakichukua
hatua za ubaguzi dhidi ya Waislamu na kuwapendelea wafuasi wa dini
nyinginezo, suala ambalo linawakasirisha sana Waislamu. Watu wengi
walikuwa na matarajio ya kupatikana mabadiliko chanya katika uwanja wa
kisiasa nchini humo baada ya kufariki dunia Meles Zenawi, Waziri Mkuu wa
zamani wa nchi hiyo, na mahala pake pamechukuliwa na Hailemariam
Desalegn. Hii ni katika hali ambayo, kamata kamata ya hivi karibuni
inayotekelezwa na serikali ya Desalegn, Waziri Mkuu wa hivi sasa wa
Ethiopia, inatajwa kuwa ni mwendelezo wa siasa za waziri mkuu
aliyemtangulia Meles Zenawi. Taasisi mbalimbali za kutetea haki za
binaadamu, zinaituhumu serikali ya Zenawi kwa kuwapendelea wananchi
wachache wakiwamo Wasomalia wa huko mashariki mwa eneo la Ogaden na
kuwafanyia ukandamizaji mkali wapinzani. Ni vyema kuashiria hapa kwamba,
Meles Zenawi alikuwa ni mwitifaki mkubwa wa Marekani na alikuwa na
ushawishi mkubwa katika mabadiliko ya kwenye nchi kama Sudan, Somalia na
kadhalika. Baada ya kuingia madarakani waziri mkuu mpya huko Somalia,
mashirika ya kutetea haki za binaadamu kwa kushirikiana na Shirika la
Kimataifa la Msamaha Duniani Amnesty International, yaliitaka serikali
ya Addis Ababa kutumia fursa iliyojitokeza, kufanya mabadiliko muhimu na
kulinda haki za binaadamu nchini humo. Aidha mashirika hayo yametaka
kusitishwa utekelezaji wa sheria ya kupambana na ugaidi iliyopitishwa na
Zenawi mwaka 2009 nchini Ethiopia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment