Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema koo na ulimi
wa wale wanaotoa wito wa umoja miongoni mwa Waislamu ni koo ya Mwenyezi
Mungu na koo na ulimi unaoibua uhasama miongoni mwa Waislamu na
madhehebu za Kiislamu ni ulimi wa shetani.
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei aliyasema hayo Jumamosi wakati
alipokutana na kufanya mazungumzo na maustadh, maqarii na mahafidh wa
Qur'ani Tukufu walioshiriki kwenye Mashindano ya 30 ya Kimataifa ya
Qur'ani Tukufu yaliyofanyika hapa mjini Tehran. Katika hotuba yake,
Kiongozi Muadhamu amesema moja kati ya maamrisho muhimu ya Qur'ani
Tukufu kwa Waislamu ni kuwataka wadumishe umoja na mashikamano.
Ameongeza kuwa kujifundisha maarifa ya Qur'ani ni jambo ambalo huandaa
mazingira ya kufikia usalama, amani, heshima na kuimarika zaidi maisha
ya Waislamu katika kivuli cha mafundisho ya Qur'ani Tukufu. Kiongozi
Muadhamu pia amesisitiza ulazima wa Waislamu kujikurubisha na kuifahamu
zaidi Qur'ani Tukufu pamoja na maarifa yake yenye kuleta saada.
Ameongeza kuwa kati ya maamurisho ya Qur'ani ni kuwataka Waislamu
washikamane kwa kamba ya Mwenyezi Mungu na wasifarakiane. Amesema
mkabala ya hilo ni njama na mbinu za mabeberu za kuibua hitilafu katika
Umma wa Kiislamu na kushadidisha taasubi za kimadhehebu. Kiongozi
Muadhamu ameashiria namna baadhi ya tawala na serikali za nchi za
Kiislamu zilivyohadaiwa na kuingia katika mtego wa adui na kusema umoja
na mshikamano wa Waislamu ni faradhi ya dharura. Kiongozi Muadhamu
amesema utawala wa Kizayuni ndio unaofaidika na umwagikaji damu na
hitilafu katika umma wa Kiislamu. Ayatullah Khamenei pia ameashiria
wimbi la chuki dhidi ya Uislamu linaloongozwa na nchi za Magharibi na
kusema adui wa Kimagharibi amewaelekezea Waislamu upanga na hivyo Umma
wa Kiislamu unapaswa kujiimarisha ili kukabiliana na hali hiyo.
No comments:
Post a Comment