Watu zaidi ya milioni moja wameandamana kote Brazil kulalamikia
viwango duni vya huduma za umma na mfumuko wa bei uliosababishwa na
maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia zitakazonfayika nchini humo
mwakani.
Polisi nchini Brazil wanasema tayari mtu mmoja amepoteza maisha katika maandaamano hayo baada ya kugongwa na gari.
Rais Dilma Roussef wa Brazil yuko chini ya mashinikizo makubwa
kufuatia maandamano hayo ambayo yameripotiwa kuwa makubwa zaidi katika
kipindi cha miaka 20 iliyopita. Bi. Roussef amelazimika kubatilisha
safari yake aliyokuwa amepanga kuenda Japan wiki ijayo.
Maandamano makubwa pia yameripotiwa katika mji mkuu Brasilia na miji
ya Rio de Janeiro na Sao Paolo. Katika mji wa Salvador polisi
walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi na risasi za plasiki
kuwatawanya waandamanaji waliojaribu kuvuruga mechi ya jana ya Kombe la
Confederations baina ya Nigeria na Uruguay. Maandamano yameanza wiki
mbili baada ya serikali kuongeza nauli. Waandamanaji sasa wamezidisha
matakwa yao na kutaka kupunguzwa kodi na bei za bidhaa muhimu. Aidha
Wabrazil wamekasirishwa na huduma duni za umma katika hali ambayo
serikali inatumia dola bilioni 26 fedha za umma kwa ajili ya maandalizi
ya Fainali za Kombe la Dunia mwakani na Michezo ya Olimpiki mwaka 2016.
No comments:
Post a Comment