Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Misri, wamefanya mazungumzo ya kina
yenye lengo la kutatua mgogoro wa Syria kwa njia za kidiplomasia.
Muhammad Kamil Amr Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Misri na mwenzake
Ali Akbar Salehi wa Iran, wamesisitizia pia juu ya udharura wa kufanyika
kikao cha Geneva 2. Mazungumzo ya viongozi hao wa Iran na Misri,
yalifanyika jana usiku kupitia njia ya simu. Kwa upande wake Waziri wa
Mambo ya Nje wa Iran amekaribisha kikao cha pande nne kilichoitishwa na
Rais Muhammad Mursi wa Misri kuhusiana na kadhia ya Syria.
Aidha
mazungumzo ya viongozi hao, yaligusia mahusiano ya pande mbili kati ya
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Misri. Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri
ametoa pongezi zake kwa taifa la Iran kwa kushiriki katika uchaguzi wa
rais uliofanyika kwa mafanikio makubwa, sambamba na kutoa mkono wa
pongezi kwa Dakta Hassan Rohani Rais Mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran kwa kuibuka mshindi katika uchaguzi huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment