Uchaguzi wa rais Venezuela unafanyika leo Jumapili huku serikali
ya nchi hiyo ikisema imevunja njama za mamuluki wa kigeni waliopanga
kuvuruga uchaguzi huo wa kumtafuta mrithi wa marehemu Hugo Chavez.
Makamu wa Rais wa Venezuela Jorge Arreaza amesema vikosi vya usalama
vimewatia nguvuni mamuliki kutoka Colombia ambao walikuwa wanapanga
kuibua ghasia katika uchaguzi wa leo. Henrique Capriles, kiongozi wa
upinzani nchini humo anayeungwa mkono na Marekani, anachuana na Nicolas
Maduro, aliyekuwa Makamu wa Rais wa hayati Hugo Chavez, na ambaye kwa
sasa ni rais wa mpito wa nchi hiyo.
Nicolas Maduro amesisitiza kuwa ataendelea kufuata siasa zile zile za
kimapinduzi za rais aliyemtangulia hayati Hugo Chavez. Maduro mwenye
umri wa miaka 50, alianza harakati zake za kisiasa wakati akiwa kijana
mdogo na kwa uungaji mkono wa harakati ya kimapinduzi inayofahamika kwa
jina la Bolivari huku akiwa dereva wa basi na kuwakilisha wafanyakazi wa
jumuiya ya usafirishaji ya mjini Caracas. Kiongozi huyo ameonya kuwa,
huduma zote za kijamii zinazotolewa kwa wasiojiweza Venezuela zitasimama
ikiwa Henrique Capriles atachaguliwa kuiongoza nchi hiyo ya America ya
Latini. Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa Maduro atamshinda Capriles
katika uchaguzi huo wa leo.
No comments:
Post a Comment