Andry Rajoelina na Marc Ravalomanana wanasiasa mashuhuri na ambao
pia ni marais wa sasa na zamani wa Madagascar kwa utaratibu wamejiondoa
katika kinyang'anyiro cha kuwania urais wa baadaye wa nchi hiyo iliyoko
katika bahari ya Hindi. Vita vya kuwania madaraka kati ya viongozi
wawili hao vilianza mwezi Machi miaka minne iliyopita na hivyo kuvuruga
utulivu wa kisiasa wa nchi hiyo. Maandamano makubwa yaliyoongozwa na
Rajoelina ambaye wakati huo alikuwa meya wa mji mkuu Antananarivo
yalimpelekea kujiuzulu Rais Marc Ravalomanana. Hata hivyo kabla ya
kuondoka madarakani Ravalomanana aliwaachia madaraka majenerali wa jeshi
ambao nao walimkabidhi madaraka hayo Rajoelina ambaye alikuwa kiongozi
wa Baraza Kuu la Mpito. Umoja wa Afrika na vyama vya upinzani
vililichukulia tukio hilo kuwa ukiukaji wa wazi wa katiba ya nchi.
Kufuatia uingiliaji kati wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
SADC, hatimaye mwezi Agosti mwaka uliopita vyama hivyo vilikubali
kugawana madaraka na Rajoelina kwa kukubali kushiriki katika serikali ya
mpito hadi wakati wa kufanyika uchaguzi mkuu mpya. Kufuatia mapatano
hayo Rajoelina aliyeongoza mapinduzi ya Machi 2009 aliteuliwa kuwa rais
wa serikali ya mpito. Licha ya hayo uchaguzi mkuu uliokuwa umepangwa
kufanyika mwaka 2011 na 2012 uliakhirishwa kutokana na tofauti
zilizojitokeza kati ya pande hasimu. Moja ya tofauti hizo zilitokana na
mjadala mkali kuhusiana na uwezekano wa kurejea au kutorejea Marc
Ravalomanana kutoka uhamishoni nchini Afrika Kusini. Ravalomanana
alihukumiwa kifo bila ya kuwepo mahakamani na mahakama moja ya mjini
Antananarivo kwa kosa la kuwaua waandamanaji walioshiriki maandamano ya
kutaka kuiangusha serikali yake. Licha ya kutolewa msamaha wa wote
nchini lakini hukumu ya mahakama hiyo ilimzuia Ravalomanana kujumuishwa
kwenye msamaha huo. Pamoja na hayo lakini SADC iliingilia kati na
kuvishawishi vyama vya kisiasa kukubali kurejea nchini Ravalomanana bila
masharti yoyote. Kwa msingi huo mpango wa mwaka 2011 uliokuwa
umekusudiwa kuleta maridhiano na umoja wa kitaifa kati ya pande hasimu
za Madagascar haukutekelezwa.
Kwa kuzingatia kwamba sasa mahasimu hao wakuu wa kisiasa wamekubali kutoshiriki katika uchaguzi ujao wa rais wa Madagascar, kuna matumaini ya kurejea tena amani na utulivu nchini humo.
Kwa kuzingatia kwamba sasa mahasimu hao wakuu wa kisiasa wamekubali kutoshiriki katika uchaguzi ujao wa rais wa Madagascar, kuna matumaini ya kurejea tena amani na utulivu nchini humo.
No comments:
Post a Comment