Uchunguzi uliofanywa na serikali ya Syria kuhusu mauaji ya halaiki ya hivi karibuni ya watu zaidi ya mia moja katika kijiji cha Houla huko magharibi mwa nchi hiyo umeonyesha kuwa makundi yanayobeba silaha yanayoipinga serikali hiyo ndiyo yaliyofanya mauaji hayo. Mkuu wa tume ya uchunguzi Brigedia Jenerali Jamal Suleiman ameeleza mbele ya waandishi wa habari kuwa magaidi waliobeba silaha ambao idadi yao ilikuwa kati ya 600 hadi 800 walitumia silaha nzito katika mashambulio waliyofanya katika kijiji cha Houla tarehe 25 ya mwezi uliopita wa Mei. Ameongeza kuwa ushahidi na uchunguzi umeonyesha kuwa watu hao wote waliouawa wakiwemo wanawake na watoto walikuwa wa familia zilizokataa kupinga serikali au kubeba silaha na ambao walikuwa na mizozo na makundi yanayobeba silaha. Aidha amesema hakukuwepo na alama zozote za uunguaji na uteketeaji wa kuashiria kwamba mashambulio ya makombora ya vikosi vya jeshi ndio yaliyosababisha maafa hayo makubwa ya roho za watu. Sulaiman aidha amesisitiza kwamba kuua watoto wadogo hakufanikishi lengo lolote la serikali bali ni makundi yanayobeba silaha ndiyo yanayofaidika na kitendo hicho. Hii ni katika hali ambayo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeielekezea serikali ya Syria kidole cha tuhuma za kuhusika na mauaji ya umati ya Houla.../
No comments:
Post a Comment