Mkutano wa 20 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika
ulimalizika jana usiku huko Addis Ababa, Ethiopia makao makuu ya umoja
huo.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Haile Mariam Desalegn ambaye pia ni
Mwenyekiti wa umoja huo amesema kwenye hotuba yake ya kufunga mkutano
huo kwamba, ulijadili kwa kina suala la amani na usalama, mapigano
yanayoendelea katika baadhi ya nchi wanachama kama Mali, Jamhuri ya
Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na mgogoro wa
kisiasa wa Madagascar.
Desalegn ameongeza kuwa, wakuu wa AU wametangaza mshikamano wao kwa
serikali ya Mali na wamesisitiza juu ya kufanyika juhudi maradufu za
kuiunga mkono serikali ya Bamako. Amesema, Umoja wa Afrika umeafiki
kutoa msaada wa dola milioni hamsini kuvisaidia vikosi vya ulinzi na
usalama vya Mali. Mkutano wa 20 wa wakuu wa Umoja wa Afrika ulianza
tarehe 27 hadi 28 ya mwezi Januari na umehudhuriwa na marais na viongozi
wa ngazi za juu wa nchi 54 za umoja huo, wawakilishi wa taasisi za
kimataifa na nchi wanachama watazamaji ikiwemo Iran.
No comments:
Post a Comment