Kwa mara ya kwanza serikali ya Zambia imewapa wafuasi wa chama
cha upinzani kibali cha kufanya maandamano katika mji mkuu wa nchi hiyo
Lusaka. Maandamano hayo yamempa Hakainde Hichilema kiongozi wa chama cha
Muungano kwa ajili ya Ustawi wa Taifa la Zambia fursa ya kunadi na
kumtaka Rais Michael Sata wa nchi hiyo aingie naye kwenye uwanja wa
mapambano ya kisiasa. Amesema katika mkusanyiko mkubwa wa wapinzani
mjini Lusaka kuwa licha ya kuwepo vitisho vya kutiwa nguvuni viongozi wa
upinzani wapinzani wataendelea kukosoa siasa za serikali. Kabla ya hapo
Hichilema alikuwa ametiwa mbaroni na sasa licha ya kuachiliwa huru
lakini bado anakabiliwa mahakamani na mashtaka ya kueneza propaganda za
uongo dhidi ya Rais Sata. Maandamano hayo ni ya kwanza kuwahi kufanywa
na wapinzani mjini Lusaka baada ya Michael Sata, ambaye ni mwanaharakati
wa kisiasa wa zamani, kuchaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo mwezi Septemba
2011.
Sata ambaye alianza harakati zake za kisiasa kwa kuteuliwa kuwa
gavana wa Lusaka ni mwanachama wa chama tawala cha zamani cha Harakati
ya Demokrasia ya Vyama Vingi MMD ambaye aliwahi kuhudumia nyadhifa
mbalimbali katika baraza la mawaziri la nchi hiyo. Aliasisi Chama cha
Taifa mwaka 2001 lakini hakufanikiwa kupata uongozi wa nchi hiyo katika
chaguzi zilizofanyika mwaka 2006 na 2008. Katika uchaguzi uliofanyika
mwaka 2011 alichuana na kumshinda Rupia Banda wa chama tawala. Ushindi
huo ulimwezesha kuhudumia nafasi ya rais wa Zambia baada ya kushindwa
mara nne katika chaguzi za kuwania nafasi hiyo huko nyuma. Ushindi wake
kimsingi ulitokana na uungaji mkono mkubwa aliopata kutoka kwa wakaazi
wa miji mikubwa. Alipata ushindi huo kupitia ahadi alizotoa kwenye
kampeni zake za uchaguzi, za kuboresha maisha ya wananchi, kuandaa
nafasi za ajira na kuimarisha viwango vya masomo kwa vijana. Licha ya
hayo wapinzani wake walimtuhumu kuwa alifanya udanganyifu kwenye
uchaguzi na kutekeleza siasa zinazipinga demokrasia. Inaonekana kuwa
maandamano ya hivi karibuni mjini Lusaka ni ishara ya kwanza ya upinzani
wa wazi wa wananchi dhidi ya serikali ya Sata. Kabla ya hapo, waungaji
mkono wake pamoja na chama tawala walijaribu kuzuia maandaamano ya
wapinzani mjini Lusaka lakini bila mafanikio. Askari usalama wameruhusu
kufanyika maandamano hayo kwa kisingizio kwamba yatapunguza hasira za
wananchi dhidi ya serikali.
No comments:
Post a Comment