
Ripoti zinasema kuwa mbali na masuala ya ukosefu wa amani na usalama, uhaba wa chakula katika maeneo ya mpaka wa Sudan na Sudan Kusini unatishia maisha ya watu wengi na kwa sasa watu laki moja na elfu 9 wanahitaji misaada ya haraka ya chakula. Inatazamiwa kuwa zaidi ya tani elfu 8 za chakula zitapelekwa katika maeneo yaliyoathiriwa na njaa huko Sudan katika wiki za hivi karibuni.
Mgogoro wa Sudan na Sudan Kusini umelitia wasiwasi pia Bunge la Ulaya. Bunge hilo limetoa taarifa likitaka kutekelezwa ramani ya njia iliyopasishwa na Umoja wa Mataifa.
Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa njama za kimataifa zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kujitokeza hali mbaya na mgogoro unaotawala maeneo ya mpaka wa Sudan na Sudan Kusini. Inaonekana pia kuwa viongozi wa Sudan Kusini ambao wamekuwa wakitumia kama wenzo na nchi za kikoloni, wanafanya juhudi za kutimiza njama za wakoloni hao kwa kuzusha hali ya machafuko na mapigano katika mpaka wa nchi hiyo na Sudan. Mfano wa wazi wa ukweli huo ni harakati za Sudan Kusini za kuanzisha mapigano na kutaka kulidhibiti jimbo la Kordofan Kusini. Mapigano hayo yamewafanya wakazi wengi wa jimbo hilo kuwa wakimbizi.
Kufuatia hali hiyo Waziri wa Ulinzi wa Sudan ametangaza kuwa nchi yake haina nia ya kufanya uhasama dhidi ya nchi jirani ya Sudan Kusini. Hata hivyo amesisitiza kuwa jeshi la Sudan liko tayari kukabiliana na uchokozi wa kigeni.
Kwa kutilia maanani hali hiyo weledi wa mambo hawana matumaini na mazungumzo yajayo kati ya pande hizo mbili ambayo yamepangwa kufanyika tarehe 21 Juni chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika.
No comments:
Post a Comment