
Waasi wa Tuareg wa kaskazini mwa Mali
Waziri wa Habari wa Serikali ya Mpito ya Mali amesema kuwa serikali hiyo inapinga hatua ya waasi wa Tuareg ya kuunda serikali huru kaskazini mwa Mali. Weledi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea nchini Mali tarehe 22 Machi mwaka huu yalichangia sana kuitumbukiza nchi hiyo katika janga la kusambaratika. Waasi wa Mali walitumia malalamiko ya wananchi na hali mbaya ya kiuchumi ya nchi hiyo kuiteka miji muhimu ya Kdal, Goa na Timbuktu ya kaskazini mwa Mali na kutangaza ukombozi wa eneo la Azawad. Hivi sasa hali bado si shwari nchini Mali, waasi wametangaza serikali mpya kaskazini mwa nchi huku Dioncounda Traore, Rais wa serikali ya mpito ya nchi hiyo akiwa ameelekea nchini Ufaransa kwa ajili ya matibabu. Itakumbukwa kuwa, wakati alipokuwa anakula kiapo cha kuongoza serikali ya mpito ya Mali, tarehe 12 Aprili mwaka huu, Traore aliwatishia waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo kwamba angelitumia nguvu za kijeshi dhidi yao. Baada ya kutoa vitisho hivyo, kundi la Ansaruddin ambalo ni miongoni mwa makundi ya waasi wa kaskazini mwa Mali lilisema kuwa liko tayari kufanya mazungumzo na serikali hiyo, lakini Traore alisema serikali haiwezi kufanya mazungumzo na waasi hao katika mazingira ya vitisho na mashinikizo. Amma kwa upande wake, wakuu wa jumuiya ya ECOWAS ya magharibi mwa Afrika wametoa mapendekezo maalumu ya kuweza kutatua mgogoro wa nchi hiyo. Mwezi Aprili mwaka huu, ECOWAS ilitoa pendekezo la kutumwa wanajeshi 2000 hadi 3000 kutoka Senegal na Gambia chini ya mwavuli wa ECOMOG kwa ajili ya kwenda kulinda amani huko Mali. Kuna uwezekano mkubwa hivi sasa serikali ya mpito ya Mali ikaiomba jumuiya ya ECOWAS iingilie kijeshi nchini humo hasa baada ya waasi wa kaskazini mwa Mali kutangaza serikali mpya. Ni jambo lililo wazi kwamba kuundwa serikali mpya na waasi wa kaskazini mwa Mali si jambo linalokubaliwa na jumuiya ya ECOWAS, lakini pia inaonekana kuwa si kazi rahisi pia kuweza kuwashinda nguvu katika kipindi kifupi waasi hao wanaoonekana kujizatiti vilivyo kwa silaha. Bila ya shaka yoyote, uingiliaji wa aina yoyote wa kijeshi nchini Mali, utaigharimu kihali na mali jumuiya hiyo ya kiuchumi ya magharibi mwa Afrika, ECOWAS.
No comments:
Post a Comment