Maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na wapinzani wa serikali ya Mauritania yamevunjwa na polisi ya nchi hiyo iliyotumia gesi ya kutoa machozi kuyavunja. Polisi ilivuruga mkusanyiko wa wapinzani waliokuwa wamekusanyika katika moja ya medani muhimu za mji mkuu Nouakchott. Ghasia zilizotokea baadaye zimepelekea watu wengi kujeruhiwa. Maandamano hayo yaliitishwa kwa pamoja na Ahmed Ould Daddah wa Republican Party for Democracy and Renewal PRDR, Ely Ould Mohamed Vall, Rais wa zamani wa Mauritania na Mohammad Jemil Mansour wa chama cha Popular Front FP.
Waandamanaji wamemtaka rais Muhammad Ould Abdul Aziz wa nchi hiyo kujiuzulu na kutoka madarakani mara moja. Wataalamu wa mambo wanasema umasikini na ubaguzi mkubwa unaoshuhudiwa katika mfumo wa utawala vimeifikisha nchi hiyo ya Kiafrika katika hatua ya kulipuka. Siku chache zilizopita kijana mmoja alijaribu kujichoma moto mbele ya bunge la seneti la nchi hiyo akilalamikia hali mbaya ya uchumi. Ukosefu wa usalama, umasikini na kuharibika uchumi ni matatizo muhimu yanayoitatiza nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo wapizani wanamtuhumu Rais Abdul Aziz kuwa hana uwezo wa kutatua matatizo hayo. Vitendo vya utekaji nyara na ugaidi vimeongezeka sana nchini Mauritania katika miaka ya hivi karibuni. Mbali na kuwa mashambulio ya kigaidi yamevuruga usalama wa Mauritania, pia yamechangia pakubwa katika kuhatarisha sekta ya utalii inayoiletea nchi hiyo na pia nchi jirani pato kubwa la fedha za kigeni. Kuenea janga la njaa katika pembe tofati za nchi hiyo ni jambo jingine ambalo limechochea ghadhabu ya wananchi dhidi ya serikali. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, zaidi ya Wamauritania milioni moja wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Linaendelea kusema kuwa idadi hiyo itaongezeka iwapo tatizo hilo halitashughulikiwa haraka. Mbali na hali mbaya ya kiuchumi, udikteta wa kisiasa nchini Mauritania ni jambo jingine linalowakera sana wananchi. Kwa kuzingatia hali hiyo, wataalamu wanasema kuwa kuna uwezekano wa kuzuka ghasia za kisiasa na matukio kama yale yaliyotokea katika nchi nyingine za kaskazini mwa bara la Afrika. Malalamiko kuhusiana na hali mbaya ya maisha na utawala mbaya katika nchi kadhaa za eneo hilo zikiwemo Tunisia, Libya na Misri yamechochea mapinduzi ya wananchi katika nchi hizo. Friday, May 4, 2012
Maandamano yafanyika Mauritania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment