Wananchi wa Bahrain wanaendelea na maandamano yao ya kupinga kuunganishwa nchi yao na Saudi Arabia. Wananchi wa Bahrain katika eneo la Sitra jana Alkhamisi walifanya maandamano makubwa ambapo sambamba na kutoa nara na sha'ar dhidi ya utawala wa Aal Khalifa walitaka vikosi vamizi vya Saudi Arabia viondoke katika ardhi ya nchi yao. Waandamanaji hao wamesema watawala wa ukoo wa Aal Khalifa watakuwa wamefanya uhaini mkubwa dhidi ya taifa la Bahrain kwa kukubali kuiunganisha nchi hiyo na Saudia, kwa sababu kitendo hicho ni sawa na kuikanyaga hati ya uhuru na kujitawala Bahrain. Wakati huohuo harakati ya al Wifaq imetoa taarifa na kuuonya utawala wa Aal Khalifa na kujiingiza katika mipango yoyote inayokinzana na mamlaka ya kujitawala na uhuru wa nchi hiyo. Taarifa hiyo ya al Wifaq imeeleza kuwa Bahrain ni nchi ya Kiarabu, ya Kiislamu na yenye kujitawala, na kwamba wananchi wake wakiwemo Mashia na Masuni wana haki na mamlaka ya kutoa maamuzi, na kwa hivyo linapokuja suala la kuingia kwenye muungano na nchi yoyote ile inapasa iitishwe kura ya maoni nchini humo. Sambamba na kuutahadharisha utawala wa ukoo wa Aal Khalifa na kujiingiza kwenye mipango ya hujuma kwa sababu tu ya kuweza kuendelea kubaki madarakani taarifa ya al Wifaq imesisitiza kwamba hatua hizo zina lengo la kuisambaratisha jamii ya Bahrain.
Katika upande mwengine Alaauddin Bourujerdi, Mkuu wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje katika Bunge la Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inaitambua Bahrain kama nchi huru na mwanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, na kwa sababu hiyo inapinga hatua ya Saudi Arabia na nchi nyengine ya kuingilia masuala ya ndani ya Bahrain ambayo ni nchi huru inayojitawala. Wakati huohuo kanali ya televisheni ya al Manar ya Lebanon imetangaza kuwa mpango wa kutaka kuiunganisha Bahrain na Saudia unalenga kuzuia wimbi la mapinduzi kutoka nchi moja hadi nyengine na kutibuka hali ya mambo katika Mashariki ya Kati. Ripoti ya kanali hiyo imeongeza kuwa kutokana na wimbi la mwamko wa Kiislamu na mapambano ya wananchi wa mataifa ya Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na nchi nyengine zilizoko chini ya tawala za kidhalimu na watawala waovu na mafisadi hususan nchini Bahrain, sambamba na kuingia hatarini maslahi haramu ya Uistikbari wa dunia, katika hali ya kuhaha na kutapatapa, madola ya kidhalimu yamezidi kuchukua ili maslahi yao haramu yasiingie hatarini zaidi. Kwa mujibu wa al Manar njama hatari ya kutaka kuiunganisha Bahrain na Saudi Arabia ni matokeo ya mpango uliobuniwa na mihimili mitatu ya Uistikbaari wa dunia yaani Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel.
No comments:
Post a Comment