Social Icons

twitterfacebookgoogle pluslinkedinrss feedemail

Thursday, May 31, 2012

Harakati ya pamoja ya waasi wa Kongo DRC dhidi ya serikali


Makundi ya waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yameamua kuunda harakati ya pamoja kwa lengo la kupigana na jeshi la serikali ya nchi hiyo. Kundi la waasi linalojulikana kama Marchi 23 kabla ya hapo lilitishia kuwa litaendelea kupambana bila kurudi nyuma na jeshi la Kongo hadi pale matakwa yake yatakapotekelezwa. Harakati ya M23 iliundwa hivi karibuni kutoka katika kundi la National Congress of Defence of the People (CNDP) ikiongozwa na Jenerali aliyeasi jeshini Bosko Ntaganda. Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na kutiwa saini miaka mitatu iliyopita kati ya kundi hilo na serikali ya Kinshasa, waasi wa CNDP waliweka silaha zao chini na kujiunga na jeshi la taifa la Kongo. Tangu mwanzoni mwa mwaka uliopita, makundi ya wanajeshi waasi yamekuwa yakidhibiti vituo kadhaa vya jeshi kulalamikia hali mbaya jeshini na kuchelewa kulipwa mishahara yao. Hivi sasa uamuzi wa makundi ya waasi ambao ni wanajeshi walioasi ya kupigana vita na jeshi la Kongo umechukuliwa katika hali ambayo, mawaziri na wabunge wa nchi hiyo wanatofautiana kuhusiana na namna ya kukabiliana na waasi hao. Baadhi ya Mawaziri na wabunge wanaunga mkono kufanyika mazungumzo kati ya jeshi na waasi katika hali ambayo wengine wanasisitiza kuendelezwa mapambano na vita dhidi ya wanajeshi hao waasi. Kwa mtazamo wa weledi wa mambo, kuwepo hitilafu na mgawanyiko kati ya mawaziri na wabunge hasa wakati huu ambapo waasi wameamua kuunda harakati ya pamoja dhidi ya serikali ni jambo hatari. Umoja na ushirikiano wa makundi ya waasi ni kengele ya hatari kwa serikali ya Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye anaiongoza nchi hiyo kwa kipindi cha pili.
Suala linalozitia wasiwasi duru za kisiasa ni kuwa, licha ya hali hiyo lakini jamii ya kimataifa imekaa kimya kuhusiana na mapigano ya Mashariki mwa Kongo bila kuchukua hatua yoyote ya kukabiliana nayo, hata baada ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa karibuni hivi kutahadharisha juu ya madhara ya kuendelea mapigano hayo katika mikoa ya Kivu Kusini na Kivu Kaskazini. Kinachohofiwa ni kwamba, huenda vita hivyo vikashadidisha mapigano kati ya makabila hasimu ya Mashariki mwa Kongo na kuifanya hali ya eneo hilo kuwa mbaya zaidi. Kwa ajili hiyo, wanaharakati wa haki za binadamu wameitaka serikali ya Congo DRC ichukue hatua za kulinda maisha na mali za watu na kuimarisha usalama wa raia ili kuzuia matatizo na kuibuka majanga katika siku zijazo. Hasa kwa kuzingatia kuwa, mgogoro wa wakimbizi wa mashariki mwa Kongo unahatarisha hali ya nchi jirani za eneo la Maziwa Makuu ya Afrika.

No comments: