![]() |
Mpita njia akipita mbele ya mabango ya kampeni za uchaguzi wa Rais Misri. |
Kesho na keshokutwa ni siku ambazo wananchi wa Misri wanatarajiwa kushiriki kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kumchagua Rais wa kwanza wa nchi hiyo tangu wananchi wampindue kibaraka mkubwa wa nchi za Magharibi, dikteta Hosni Mubarak.
Kampeni za uchaguzi zilimalizika jana Jumatatu nchini humo na huo unatarajiwa kuwa uchaguzi wa kihistoria hasa kwa vile Wamisri wamepitisha makumi ya miaka bila ya kuwa na uchaguzi huru wa Rais.Wagombea 13 wa mirengo tofauti wanachuana kwenye kinyang'anyiro hicho ambapo katika kipindi hiki cha baina ya kumalizika kampeni za uchaguzi hadi wakati wa uchaguzi wenyewe, mgombea yeyote yule hana ruhusa ya kujitokeza kwenye televisheni au kufanya mazungumzo na vyombo vya habari wala kufanya jambo lolote lile la kuvutia wapiga kura.
Abul Futuh pamoja na mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Amr Moussa na mgombea wa kundi la Ikhwanul Muslimin, Muhammed Mursi, ndio wagombea wakuu katika uchaguzi huo wa kihistoria.
Mgombea wa Ikhwanul Muslimin, Muhammed Mursi ndiye aliyepata kura nyingi za Wamisri waishio nje ya nchi. Uchaguzi huo wa rais wa Misri ulianza rasmi siku ya Ijumaa ya tarehe 11 mwezi huu wa Mei kwa Wamisri walioko nje kupiga kura katika balozi za nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment