Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa
(Unicef) umeeleza kuwa watoto wengi walionusurika kifo wakiwa katika
safari ngumu kwenye bahari ya Mediterania wakitokea Libya kuelekea
Italia hawakuongozana na watu wazima; na hivyo kuwafanya watoto hao kuwa
katika mazingira ya kuweza kukabiliwa na vitendo vya unyanyasaji na
kutumiwa kama watumwa.
Sarah Crowe, Msemaji wa Unicef amesema kuwa asilimia 92 ya
watoto 7,600 ambao walivuka bahari ya Mediterania katika mazingira
hatari kati ya Januari na Mei mwaka huu hawakuwa na wazazi au ndugu zao.
Ameongeza kuwa wengi wa watoto hao walikuwa wavulana wenye umri kati ya
miaka 15 na 17 kutoka Somalia, Nigeria na Eritrea.
Msemaji wa Unicef ametahadharisha kuwa wavulana na wasichana hao
ambao waliwasili Ulaya wamekabiliwa na vitendo vya ukahaba, magenge ya
udhalilishaji wa kijinsia na uhalifu. Itakumbukwa kuwa mwezi Februari
mwaka huu wakala wa Umoja wa Ulaya wa Europol uliripoti kuwa watoto
wakimbizi zaidi ya 10,000 ambao hawakuwa na wazazi au jamaa walipotea
katika wimbi la wakimbizi la hivi karibuni kuelekea Ulaya.
No comments:
Post a Comment