Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah nchini Yemen amesema kuundwa
Baraza la Taifa la Mpito ni hatua inayoweza kuvunja njama zote na kujaza
pengo la kisiasa katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Akizungumza katika kikao cha hadhara siku ya Jumamosi Abdul-Malik
al-Houthi amesema kuna baadhi ya madola ya kigeni ambayo yamechochea
kujiuzulu rais Abd Rabbu Mansur Hadi na waziri mkuu Khaled Bahah kwa
lengo la kuibua pengo la kisiasa na kuvuruga taasisi za kiserikali.
Hatahivyo kiongozi huyo wa Harakati ya Ansarullah amesema watu wa Yemen
wana azma ya kufikia malengo hayo halali. Aidha amesema mlango wa
ushirikiano na umoja uko wazi kwa makundi yote ya kisiasa nchini humo.
Siku ya Ijumaa Harakati ya Ansarullah ilitangaza kuundwa Baraza la
Taifa la Mpito. Kwa mujibu wa tangazo hilo wanamapinduzi wa Ansarullah
wamelivunja bunge na kutangaza uundwaji wa baraza la rais lenye wajumbe
watano litakalofanya kazi kama serikali katika kipindi cha mpito cha
miaka miwili. Tangazo hilo la katiba aidha limeongeza kuwa baraza la
taifa la mpito lenye wajumbe 551 ambalo litachukua nafasi ya bunge
litaundwa ili kuchagua baraza la rais katika jitihada za kumaliza mkwamo
wa kisiasa ambao umekuwa ukishuhudiwa nchini Yemen.
No comments:
Post a Comment