Marekani imeiomba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran isaidie katika
kutatua hali ya mambo nchini Iraq. Jen Psaki, Msemaji wa Wizara ya Mambo
ya Nje ya Marekani ameyasema hayo leo katika kikao na waandishi wa
habari mjini Washington wakati akijibu swali la mwandishi mmoja wa
habari kuhusiana na nafasi iliyonayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika
kuisaidia Iraq kiulinzi dhidi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi
linalojiita Dola la Kiislamu la Iraq na Sham 'DAESH', ambapo amesema
kuwa, anataraji kuiona Tehran ikisaidia kurejesha hali ya amani nchini
Iraq.
Psaki anatoa matamshi hayo katika hali ambayo Waziri wa Mambo ya Nje
wa Russia, Sergey Lavrov amesema kuwa kile kinachojiri nchini Iraq ni
matokeo ya uingiliaji kijeshi wa Marekani na Uingereza katika nchi hiyo
ya Kiarabu. Naye kwa upande wake Aleksey Pushkov, Mkuu wa Kamisheni ya
Mambo ya Kimataifa katika bunge la Russia, amesema kuwa Marekani ni
muhusika wa hali ya sasa nchini Iraq na mashambulizi yanayoendelea
nchini humo. Pushkov amesema kuwa, uvamizi wa Marekani na Uingereza
nchini Iraq miaka 10 iliyopita, ndio sababu iliyochangia makundi ya
kigaidi kuweza kuudhibiti mkoa wa Mosul na maeneo mengine ya nchi hiyo.
Amesema kuwa, uvamizi wa Marekani kuanzia mwaka 2003 hadi 2011 nchini
Iraq, ulitekelezwa kwa lengo la eti kupambana na makundi ya kigaidi,
katika hali ambayo hii leo inashuhudiwa kuwa, matunda ya uvamizi huo
ilikuwa ni kuzalisha zaidi makundi hayo ndani ya taifa hilo. Wakati huo
huo, duru za habari nchini Iraq zinaeleza kuwa, wanamgambo wa Daesh
wameanza kukimbia kutoka mjini Mosul kufuatia mashambulizi makali ya
anga yanayofanywa na jeshi la nchi hiyo dhidi ya wanamgambo hao. Kwa
mujibu wa habari, wapiganaji wa Daesh wameondoka katika barabara za mji
huo na kukimbilia eneo la Rabia, kufuatia mashambulizi makali ya anga ya
jeshi la Iraq.
No comments:
Post a Comment