Mkuu wa jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Jenerali
Benny Gantz amekiri kuwa, hivi sasa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya
Hizbullah nchini Lebanon, ni jeshi la saba kwa nguvu duniani ambapo
inamiliki makombora ambayo yanaweza kuyafunika maeneo yote ya utawala
huo. Akiashiria uwezo wa harakati hiyo dhidi ya utawala wa Kizayuni,
Gantz amesema kuwa, uwezo wa nguvu za Hizbullah unazizidi nchi nyingi
zilizoendelea duniani.
Jenerali Benny Gantz ameyasema hayo katika kikao cha mwaka cha
Herzliya ambacho kinawakutanisha wakuu wa kisiasa na usalama wa utawala
huo bandia ambapo alisema kama ninavyomnukuu: "Nitajieni majina manne au
matano ya nchi kubwa zenye uwezo wa kijeshi kama iliyonayo harakati ya
Hizbullah huwezi kuzikuta isipokuwa ni Marekani, China, Russia, Ufaransa
na Israel." Mwisho wa kunukuu. Ameongeza kuwa, hivi sasa Hizbullah
inaendesha mapambano katika pande tatu tofauti na kwamba kuna uwezekano
wa kushinda kwa uzoefu wake.
Hata hivyo Jenerali Gantz hakuweka wazi ni mapambano gani hayo matatu
yanayoendeshwa na Harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah
nchini Lebanon. Itakumbukwa kuwa, mwaka jana afisa huyo wa jeshi la
utawala haramu wa Kizayuni alionya kwamba hatua ya wapiganaji wa
Hizbullah kushiriki katika vita nchini Syria, inawaongezea uwezo wa hali
ya juu na uzoefu wa kijeshi wapiganaji hao wa harakati hiyo dhidi ya
utawala huo wa Kizayuni.
No comments:
Post a Comment