Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, limeonya juu ya hali
mbaya ya kibinaadamu nchini Sudan Kusini. Shirika hilo lenye makao yake
mjini Geneva, sambamba na kutoa ripoti kuhusiana na suala hilo limesema
kuwa, hali ya kibinaadamu nchini humo ni ya hatari na kuongeza kuwa,
hali imekuwa mbaya zaidi katika kipindi hiki kufuatia kuanza kunyesha
kwa mvua ambazo kwa mujibu wa shirika hilo, zitakwamisha zoezi la
kufikisha misaada ya kibinaadamu kwa waathirika wa mgogoro nchini humo.
Aidha shirika hilo limesisitiza kuwa, tangu kuanza kwa mgogoro nchini
Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka jana, zaidi ya watu laki mbili na elfu
50 wameshapokea misaada ya shirika hilo. Wakati huo huo mkuu wa timu ya
shirika la Msalaba Mwekundu nchini Sudan Kusini amesema kuwa, hadi sasa
hali ya mambo nchini humo bado ni mbaya na kwamba, ikiwa misaada
haitawafikia wahusika haraka, basi kuna uwezekano wa kuongezeka uhaba wa
chakula ndani ya nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Kwa upande mwingine Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu,
limezitaka pande zinazopigana nchini Sudan Kusini kutekeleza ahadi zao
kwa mujibu wa sheria za kimataifa ili kuiepusha nchi hiyo na umwagikaji
damu zaidi.
No comments:
Post a Comment