Muungano wa Jubilee unaoongoza serikali ya Kenya
umeketaa takwa la muungano wa upinzani ujulikanao kama Cord la kutaka
mazungumzo ya kitaifa yafanyike siku ya Julai Saba maarufu kama Saba
Saba.
Akizungumza baada ya mkutano wa wabunge na maseneta wa
Jubilee katika Ikulu ya Rais mjini Nairobi, Kiongozi wa Waliowengi
katika Bunge la Taifa la Kenya, Aden Duale, amesema, mazungumzo yoyote
ya kitaifa yanapapswa kufanyika kupitia taasisi zilizoundwa kikatiba.
Ametoa mfano kuwa, ramani ya kuvunjwa Tume Huru ya Uchaguzi IEBC iko
wazi kabisa katika katiba na kwamba rais wa nchi na serikali huhusika na
kadhia hiyo baada ya mkondo wa bunge kumalizika. Duale ameendelea
kusema kuwa vinara wa Cord, Raila Odinga na Kalonzo Musyoka wanaweza
kukutana na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu.
Viongozi wa Cord walihutubia mkutano mkubwa wa hadhara
mjini Nairobi wakati wa kumkaribisha kinara wao Raila Odinga aliporejea
kutoka safari ya miezi mitatu Marekani. Katika mkutano huo wakuu wa Cord
walitaka mazungumzo ya kitaifa yafanyike ili kujadili changamoto muhimu
zinazoikabili Kenya kama vile usalama, ufisadi, uteuzi katika nafasi za
umma, mfumo wa uchaguzi na marekebisho katika mfumo wa ugatuzi.
No comments:
Post a Comment