Ismail Haniya, Waziri Mkuu wa serikali halali ya Palestina
amesisitiza kuwa, tofauti zilizoko kati yake na Rais wa Mamlaka ya Ndani
ya Palestina, Mahmoud Abbas, kamwe hazitovuruga makubaliano ya
maridhiano ya kitaifa licha ya kuwa tofauti hizo hadi sasa
zimechelewesha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa. Makubaliano hayo
kati ya Fat'h na HAMAS yalisainiwa mwezi Aprili na moja ya vipengee
muhimu ni kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa itakayoyashirikisha
makundi yote ya Palestina.
Licha ya Mahmoud Abbas kumteua Waziri Mkuu wake wa sasa,
Rami Hamdallah, kuwa kiongozi wa serikali hiyo ya umoja wa kitaifa, bado
kuna mambo mengi yanayokwamisha kutangazwa baraza jipya la mawaziri
huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.
Wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje ni moja kati ya mambo yanayoendelea
kuzusha utata kati ya Fat'h na HAMAS na hivyo kuchelewesha uundwaji wa
serikali mpya. Mahmoud Abbas anashinikiza kuteuliwa Riyadh al-Maliki
kushikilia wadhifa huo lakini Hamas imepinga mashinikizo hayo. Pia
Harakati ya HAMAS imepinga kuvunjwa Wizara ya Wafungwa ikisema hatua
hiyo itatoa pigo kubwa la kisaikolojia kwa wafungwa wa Kipalestina
wanaoendelea kuteseka kwenye jela za Wazayuni.
Wachambuzi wengi wanatiwa wasiwasi na kuendelea kujitokeza
tofauti nyingi kati ya Fat'h na HAMAS na wanaitakidi kuwa suala hilo
linayumbisha na kuhatarisha makubaliano ya maridhiano ya kitaifa ya
Aprili 23.
Hapana shaka kwamba, kuungana na kushirikiana Wapalestina
ndiyo njia pekee ya kukabiliana na njama za Wazayuni na waitifaki wao wa
Magharibi wakiongozwa na Marekani. Kusimama pamoja Wapalestina
kutawasaidia kudai na kupigania haki zao na uwezekano mkubwa ni kwamba
watashinda kwenye mapambano hayo wakiwa kitu kimoja. Ni kutokana na
kumaizi ukweli huo, ndio maana Wamarekani na Wazayuni wameanzisha fitna
kubwa kujaribu kuyagonganisha vichwa makundi ya Wapalestina ili
yasifikie lengo lao kuu la kuungana. Miongoni mwa njama za Wazayuni na
Wamarekani ni kumtumia Mahmoud Abbas kwa kujaribu kumvuta tena kwenye
mazungumzo na Wazayuni wakijidai kwamba wamekubali kulegeza kamba kwenye
baadhi ya misimamo yao ya wali.
Kwa bahati mbaya, Mahmoud Abbas anaonekana kuchanganyikiwa
na kuyumba kwenye misimamo yake licha ya kuahidi kwamba atafungamana na
makubaliano ya maridhiano ya kitaifa ya mwezi Aprili. Baadhi ya weledi
wa mambo wanaamini kuwa, huenda Abu Mazin anatumia kadhia ya umoja wa
Wapalestina kama karata ya turufu kupima misimamo ya Wamarekani na
Wazayuni na kuwalazimisha kulegeza kamba katika baadhi ya mambo.
Wachambuzi hao wanasema si ajabu kwa Abbas kujiondoa kenye makubaliano
na HAMAS na kurudi tena kwenye meza ya mazungumzo eti ya amani na
Wazayuni iwapo ataona maslahi yake yanadhaminiwa na kulindwa kwa njia
hiyo. Hatua ya Abbas ya kumteua Riyadh al-Maliki ambaye tangu mwanzoni
ana matatizo na wanachama wa HAMAS ni miongoni mwa harakati za kiongozi
huyo za kuchafua anga ya maridhiano kati ya makundi ya Kipalestina.
Alaa kulli hali, kuyumba misimamo ya Mahmoud Abbas mkabala
wa maridhiano ya kitaifa kumekosolewa na Wapalestina wengi wanaohofia
kwamba fursa iliyojitokeza ya kuungana yumkini ikapotea tena na hivyo
kuwapa nguvu Wazayuni kushadidisha hujuma, jinai na dhulma zao za kila
siku dhidi yao.
No comments:
Post a Comment