Gazeti la Daily Telegraph linalochapishwa nchini Uingereza
limeandika ripoti inayoonyesha kupanuka satua na wigo wa makundi ya
kigaidi barani Afrika. Ripoti hiyo iliyochapishwa kwenye toleo la leo
Alhamisi inasema kuwa, makundi ya kitakfiri na yale yenye misimamo ya
kufurutu ada ambayo yana mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda
yameendelea kuenea kwa kasi na kuwa na ushawishi mkubwa barani Afrika.
"Tangu kuuawa Osama bin Laden mwaka 2011, matawi ya al-Qaeda yamepungua
mno katika Peninsula ya Arabia na yanaonekana kuhamia barani Afrika"
inasema sehemu moja ya ripoti hiyo. Daily Telegraph limetaja makundi
kama vile, al-Shabab la nchini Somalia, Boko Haram la nchini Nigeria na
AQIM katika nchi za Algeria, Mali na Niger na kusema kuwa, udhaifu wa
serikali za Afrika umetoa mwanya kwa makundi hayo kuendesha harakati zao
bila woga.
Huku hayo yakijiri, Serikali ya Uingereza imetahadharisha kwamba,
kuna uwezekano wa kushambuliwa Djibouti na kundi la kigaidi la al-Shabab
la nchini Somalia. Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza huku ikiashiria
kuwa taarifa za kiintelijensia ilizopata kuhusu mipango ya al-Shabab ni
za kweli, imewataka raia wake walioko Djibouti kuondoka nchini humo au
kuchukua tahadhari ya hali ya juu.
No comments:
Post a Comment