Mawaziri wa Fedha wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wamesoma
bajeti za nchi zao mbele ya wabunge leo alasiri. Bajeti hizo
zinazoainisha jinsi serikali za nchi hiyo zitakavyotumia fedha za umma
katika mwaka 2014/2015 zimetoa vipaumbele tofauti kutoka nchi moja hadi
nyingine.
Nchini Kenya, Waziri wa Fedha, Henry Rotich amesoma bajeti ya
Shillingi Trilioni 1.8 ambapo sekta za Elimu na Usalama wa Taifa ndizo
zilizopata kiwango kikubwa cha fedha.
Akisoma bajeti hiyo mbele ya
wabunge, Waziri Rotich amesema wizara yake imeamua kutoa kipaumbe cha
kwanza kwa elimu kutokana na ahadi ya serikali ya kuboresha sekta hiyo
kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu nchini. Waziri huyo amesema bajeti
inatazamiwa kukua hadi asilimia 6.8 mwaka ujao wa 2015.
Huko Uganda, Waziri wa Fedha, Maria Kiwanuka amesoma bajeti ya
Shilingi trilioni 14 ambapo sekta za kazi na uchukuzi ndizo zilizopata
kitita kikubwa cha fedha. Waziri Kiwanuka amesema serikali ya Kampala
ina nia ya kurahisisha usafiri wa bidhaa na watu ndani na nje ya Uganda
na kwa mantiki hiyo imeonekna pana haja ya Wizara ya Uchukuzi kutengewa
fedha zaidi. Bajeti ya mwaka uliopita ya Uganda ilikuwa ya trilioni 13.1
Bajeti ya Rwanda imetajwa kuwa ya Franga trilioni 1.75 ambapo Waziri
wa Fedha, amesema nchi hiyo inakabiliwa na nakisi ya bajeti ya Franga
bilioni 177.2. Kiwango kikubwa cha nakisi hiyo kitajazwa kutokana na
mikopo ya ndani na nje ya nchi.
Mjini Dodoma, Tanzania, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, amesoma Bajeti
ya zaidi ya shilingi trilioni 19 ikiwa ni takriban asilimia 7 zaidi
ikilinganishwa na ile ya mwaka uliopita ya trilioni 18.2. Waziri Saada
Mkuya amesema serikali itafunga mianya inayotumiwa na wakwepaji kodi ili
kukusanya kodi ya kutosha pamoja na kuweka mikakati itakayoleta nidhamu
katika matumizi ya fedha za umma. Hii ni katika hali ambayo, Tanzania
imekumbwa na kashfa kadhaa za ufisadi na utumiwaji mbaya wa fedha za
umma katika kipindi cha miezizi sita iliyopita.
No comments:
Post a Comment